Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema sekta ya afya ni amesema Sekta hiyo ni nyeti na kwa unyeti wake lazima kuzingatiwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Ameyasema hayo leo Julai 06, 2024 wakati wa Kongamano la kitaifa la wadau wa Sekta ya Afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Sekta ya afya ni sekta nyeti sana na inamgusa kila mtu, kwahiyo tukaona tukutane tujadili kwa pamoja afya tuitakayo 2050.
“Changamoto kubwa ambayo tunakabiliana nayo kwasasa hivi ni gharama za matibabu zimepanda, lakini tunaamini msingi tumeshauweka wa kutatua changamoto hiyo kwa kuanzisha kwa bima ya afya kwa wote,” amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo amewataka Watanzania kubadilka na kuwekeza katika afya kwa kuhahakisha wanakuwa na bima za afya.
“Ndugu zangu watanzania kama kila mmoja wetu akiguswa na kuchangia huduma za Bima ya Afya ni dhahiri shahiri kuwa huduma zetu zitaboreka. Tusingoje mgonjwa yupo, Muhimbili, JKCI, Bugando au mahala pengine ndio uanze kukimbizana na Bima ya Afya, hakuna Bima ya hivyo, tuzingatie miongozo na Sheria inavyotaka” amesema Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema, Wizara ya Afya imefanya vizuri katika Dira ya 2000/2025 inayomaliza muda wake katika masuala mbalimbali ya kukabiliana na baadhi ya magonjwa ya mlipuko kama Covid 19.
“Tumefanikiwa sana, juu ya suala la wanawake kujifungulia katika Vituo vya Afya, kwani imeongezeka kutoka asilimia 41 mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 81 kwa sasa na tutajitahidi ifikapo 2025 tuwe tumefikia asilimia 100.
“Tumewafikia watoto 94 kati ya watoto 100 katika suala zima la Chanjo hii inatupatia morari na tutahakikisha malengo yanatimia ifikapo 2025 kwakuwafikia watoto 100” amesema Waziri Ummy.