Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

TUME ya Ushindani nchini (FCC) imeendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuhusu bidhaa bandia katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo katika viwanja vya maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa FCC, William Erio amesema FCC itahakikisha mwananchi yeyote haumizwi na bidhaa zisizo na ubora ikiwemo kusimamia sheria ya ushindani nchini inayodhibiti bidhaa hizo.

Aidha Erio amesema FCC imejitahidi kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya kuepuka bidhaa bandia.

“Majukumu yetu pia ni kutoa elimu kwa watu kutokufanya Biashara Bandia na kuharibu ushindani wa biashara, sisi FCC tutaendelea kuchukua hatua kwa yeyoye atakayebainika kufanya hivyo,”amesema Erio.

Pamoja na hayo amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kabla ya kufanya biashara nchini watembelee FCC kwa lengo la kupata elimu .

“Na sisi tunatumia maonesho haya pamoja na kueleza kazi kwa Umma,tunatumia maonesho haya pia kunawashauri kutofanya Biashara Bandia pamoja kutoweka bei kubwa itakayomuumiza mlaji,”

“Tunawakaribisha kwenye Banda hili, tutatoa elimu kipindi chote cha maonesho, hivyo niwakaribishe Wafanyabiashara na wananchi Kwa ujumla waweze kutembelea banda letu,” amesema Erio.

Hata hivyo, amewahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ni sehemu sahihi kwa uwekezaji kutokana na sera nzuri ikiwemo kuwepo kwa Mamlaka inayodhibiti bidhaa bandia.

Please follow and like us:
Pin Share