Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma
Jeshi la Polisi Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma linamshikilia Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Wilayani humo Irving Mutegeki kwa tuhuma za kukutwa na meno ya Tembo.
Mutegeki Bagasheki amekamatwa na nyara hizo za Serikali Wilaya ya Kibondo Julai 2,2024 akiwa kwenye gari binafsi majira ya usiku na anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Meneja huyo wa TRA anadaiwa amekuwa akifanya biashara ya meno ya Tembo kutoka Wilaya ya Kibondo na Kakonko kwenda mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi ikiwemo Burundi.
Hata hivyo kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa za mauaji ya Tembo katika misitu na hifadhi zilizopo katika wilaya ya Kibondo na Kakonko.
Taarifa kutoka Wilayani humo inaonyesha kuwa kuna jitihada za kuficha suala hilo kwa kutengenezwa mazingira ya rushwa ili kulimaliza jambo hilo ambalo ni uhujumu uchumi.