Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

IMEELEZWA kuwa, Tanzania sasa ipo tayari kwa matumizi ya teknolojia ya Akili Mnemba na kwamba Watanzania hawapaswi kuwa na hofu yoyote, kwani teknolojia hiyo haiji kuondoa nafasi za kazi bali kuongeza tija.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga wakati akifanya wasilisho kuhusu “Utayari wa Tanzania kwa Akili Mnemba na Mustakabali wa Kazi” hivi karibuni wakati wa mkutano mkuu wa 65 wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) jijini Dar es Salaam.


Alisema; “Akili Mnemba haijaja kuondoa nafasi za wafanyakazi, bali itabadilisha ufanyaji kazi na hivyo kuongeza tija.”
Aliongeza kuwa, kitakachofanywa na teknolojia ya Akili Mnemba ni kubadilisha namna ya ufanyaji wa kazi, hivyo Watanzania wanapaswa kujiongezea ujuzi na kujifunza fani mpya zinazokuja na zama hizi za Akili Mnemba au Akili Bandia.

Alitoa mfano wa fani kama za wataalamu wa uendeshaji roboti (Robot Coordinators), Wafunza mifumo ya kujifunza mashine (Machine Learning Trainers), Wataalamu wa Maadili wa AI (AI Ethicist), Wabunifu wa Chatboti (Chatbot designers), Wataalamu wa Ufundi wa Afya Endeshwa na AI (AI powered Healthcare Technician).

Katika kuonesha utayari wa Tanzania, Dkt. Mwasaga alisema kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijiti (DTP), kwa mara ya kwanza Tanzania itakuwa mwenyeji wa kwanza wa kilele cha Shindano la Ubunifu barani Afrika la vijana kwenye masuala ya Akili Mnemba na Roboti wakati wa Kongamano la Nane la Wataalamu wa TEHAMA Tanzania (TAIC) litakalofanyika kwa siku tano kuanzia Oktoba 13, jijini Dar es Salaam.

Shindano hilo la teknolojia ibukizi linaungwa mkono na Umoja wa Afrika (AU) inayolenga kukuza matumizi sahihi ya Akili Mnemba na Roboti kwa vijana barani Afrika. Itatoa zawadi ya Dola za Kimarekani 100,000 (Zaidi ya Shilingi milioni 250 za Kitanzania) kwa washindi.

Tume ya TEHAMA huandaa Kongamano hilo la kila mwaka ikiwa ni sehemu ya jukumu lake la kuwezesha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA pamoja na sera nyingine zinazohusiana na kuendeleza matumizi ya TEHAMA nchini kama vile kukuza na kuvutia uwekezaji wa TEHAMA nchini ili kuwezesha kutengeneza ajira na kuchangia katika shughuli za kiuchumi na kijamii; lakini pia kuimarisha uratibu wa shughuli za TEHAMA ili kuongeza mchango wa TEHAMA katika uchumi wa taifa.

Akisisitiza umuhimu wa Akili Mnemba, Dkt. Mwasaga amezipongeza taasisi za Umma zinazochangamkia matumizi ya teknolojia ibukizi, akitolea mfano wa Mahakama ya Tanzania ambayo imeshaanza kutumia Akili Bandia kuendesha na kuratibu mashauri katika Mahakama mbalimbali nchini, hatua itakayochochea uharakishaji wa utoaji wa haki kwa wananchi.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel Aprili mwaka huu alithibitisha taasisi yake kujikita katika matumizi ya Teknolojia, akisema kutokana na umuhimu ya sekta hiyo, Mahakama imeshaanza matumizi hayo na ifikapo mwaka 2025 kazi zake zote zitakuwa zikifanywa kwa mtandao.

“Kama mnavyofahamu hivi karibuni tumeanzisha mfumo wa akili bandia kama mtakumbuka vizuri tuna kile kitu kinaitwa (artificial intelligency/ akili mnemba) tumekuwa taasisi ya kwanza kutumia artificial intelligence maana yake ni kwamba sasa ile hukumu ambayo jaji au hakimu alikuwa anaandika kurasa 200 sasa anaongea tu akimaliza kuongea anabonyeza kitufe na kinaanza kutafsiri kwa lugha mbalimbali, hivyo kazi za Mahakimu na Majaji itakuwa ni ndogo tu nayo ni kutoa maamuzi,” alisema.

Kwa hatua za majaribio, Akili Mnemba imeshaanza kutumika katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala Kuu, Kituo Jumuishi cha Masula ya Familia Temeke. Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Kinondoni na sasa usimikaji wa miundombinu hiyo wezeshi unaendelea katika Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki Arusha, Mwanza, Morogoro, Dodoma, Mahakama Kuu Kanda ya Musoma na Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.