Rais wa Kenya William Ruto amesema kuwa “hana hatia” na vifo vya waandamanaji vilivyotokea mapema wiki iliyopita katika maandamano ya kuipinga serikali yake.
Ruto ametoa kauli hiyo wakati mamia ya watu wakikusanyika jana katika mji mkuu wa Nairobi kuwakumbuka watu waliouawa kwenye maandamano yaliyogeuka kuwa ya vurugu.
Katika mahojiano na kituo kimoja cha cha televisheni cha Kenya, Rais Ruto amesema idadi ya watu waliokufa ni 19, ikiwa ni takwimu za kwanza kutolewa na mamlaka. Rais Ruto aidha ameahidi uchunguzi kamili kuhusiana na vifo vya waandamanaji.
Mashirika ya haki za binadamu yamesema kuwa watu wasiopungua 30waliuawa katika maandamano yaliyochochewa na dhamira ya serikali ya kutaka kuongeza ushuru kupitia muswada tata wa fedha wa 2024.
Kufuatia machafuko yaliyojitokeza, Rais Ruto alibadili msimamo wake akisema kuwa “atawasikiliza watu” na hatosaini muswada huo kuwa sheria.
Polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji waliovamia majengo ya bunge na kuchoma moto. Akizungumzia vifo vya waandamanaji, Ruto alisema kuwa “Ni kwa bahati mbaya. Kama demokrasia hayo hayapaswi kuwa sehemu ya mazungumzo yetu”.
Ameongeza kuwa polisi walifanya kila waliloweza, na kama “kulikuwa na matumizi ya kupita kiasi, tunazo nyenzo za kuhakikisha tunashughulikia hilo. Afisa yeyote muuaji ambaye alienda zaidi ya ilivyoainishwa kwenye sheria atachukuliwa hatua,” alisema Ruto.
Lakini ameonya kwamba wale waliovamia bunge pia watawajibishwa. “Wale waliovamia bunge na mahakama wamenaswa katika CCTV”.
Akizungumzia uamuzi wa kuachana na muswada huo wa fedha dakika za mwisho, Ruto alisema kwamba hiyo inamaanisha wamerudi nyuma karibu miaka miwili na serikali itapaswa kukopa kwa uzito. Aidha kiongozi huyo amekiri kwamba kama serikali walipaswa kutoa maelezo ya kina kuhusu muswada huo.
“Nikipewa nafasi ya kueleza watu wa Kenya muswada wa fedha ulikuwa unahusu nini na ungewafanyia nini, basi kila Mkenya angekubaliana nami.”Rais wa Kenya asema yuko tayari kuzungumza na Gen-Z
Siku ya Jumamosi, baadhi ya watu walikusanyika katika bustani ya Uhuru katikati mwa Nairobi. Baada ya kuimba na kuwasha mishumaa, walipeperusha bendera ya Kenya na kupita katika hospitali ambako baadhi ya majeruhi bado wanatibiwa.