Profesa Mohamed Janabi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Daktari bingwa na Mbobezi kwenye magonjwa ya moyo amewasili mkoani Arusha usiku wa Jumatano Juni 26, 2024 tayari kuhudumia wananchi kwenye Kambi maalum ya Matibabu inayoendelea mkoani Arusha kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid.
Prof. Janabi ni miongoni mwa Madaktari wanaoheshimika nchini Tanzania na mwenye uzoefu wa hali ya juu katika utabibu na taaluma yake, akitoa mchango mkubwa katika kushauri masuala ya afya pamoja na maboresho ya huduma za afya na ustawi wa jamii, akijitolea pia katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa lishe na mtindo bora wa maisha.
Mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro KIA, Profesa Janabi amesema akiwa Arusha atakuwa na majukumu makuu mawili, kupima na kutibu wananchi wa Arusha pamoja na kutumia muda wake kuelimisha jamii dhidi ya magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ambayo anasema yanawatesa watu wengi zaidi na kusababisha vifo vya watu wengi.
Tayari timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wamekuwepo kwenye kambi hiyo tangu Jumatatu ya wiki hii na kuongezeka kwa Prof.Janabi ni mwanzo wa ahadi ya Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ya kuongeza idadi ya madaktari kwenye kambi hiyo ili kuongeza kasi na ufanisi katika huduma za vipimo, matibabu na elimu ya afya ya jamii.