Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato
SERIKALI imezitaka taasisi zisizokuwa za kiserikali kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, rushwa, ngono, dawa za kulevya, mauaji pamoja na mimba za utotoni hasa kwa kundi balehe.
Hatua hiyo inatokana na jamii kupoteza misingi ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto ,jambo linalosababisha baadhi ya na vijana kujiingiza katika vitendo viovu ikiwemo ushirikina na mauji ya watu wasiokuwa na hatia.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, mkoani Geita, Said Nkumba, amesema hayo wakati akifungua mkutano mkuu wa sita wa mtandao wa walimu walezi wa Club za wanachama wa FEMA nchini unaofanyika wilayani hapa kwa siku tatu.
Katika ufunguzi huo, DC Nkumba amelipongeza shirika lisilo la kiserikali la Femina kwa kutimiza miaka 25 ya uwepo wake katika utoaji wa elimu kwa vijana na miaka 22 ya jarida la FEMA ambalo limekuwa likitoa mafunzo mazuri kwa vijana walioko shule za sekondari na vyuo mbalimbali nchini.
Naibu Mkurugenzi mkuu wa Femina Tanzania, Amabilis Batamula, amesema uwepo wa taasisi hiyo umesaidia vijana wengi kujitambua, kujilinda na kujithamini na kwamba ili jamii iweze kufikia haraka maendeleo yanayokusudiwa ni muhimu kuwa na jamii iliyostaarabika.
Hata hivyo amesema mkutano huo unalenga kubadilishana mbinu,uzoefu na maarifa kwa walimu walezi wa club za Fema shuleni hatua itakayosaidia kuinua taaluma na kupunguza suala la mimba za utotoni,ubakaji,ulawiti na utumiaji wa dawa za kulevya kwa vijana.
Kaimu mwenyekiti wa mtandao wa walimu walezi wa club za Fema nchini, mwalimu Benjamin Mhanda,amesema wazazi,viongozi na walimu bora wa baadaye wanapaswa kuandaliwa sasa na kwamba hakuna njia ya mkato katika suala zima la maadili isipokuwa ni jamii kuelimishwa na kupewa taarifa sahihi na kwa wakati.
“Tumekutana hapa kwa lengo la kujengeana mbinu mbalimbali tutakazotumia katika malezi ya vijana wetu mashuleni,istoshe kundi kubwa la vijana lipo shuleni na siye ndiyo tunashinda nao muda mrefu kuliko wazazi”amesema Mhanda.
Mwalimu Joyce Haule,kutoka Kilindi anasema uwepo wa club za Fema mashuleni unasaidia vijana kujifunza masuala mazima ya Balehe na namna wanavyoweza kukabiliana na hali hiyo pasipo kufanya ngono,kujitambua, kujithamini,kujipenda,pamoja na namna wanavyoweza kutoa taarifa ya masuala ya ukatili katika jamii inayowazinguka.
Kadhalika hutambua mambo mbalimbali katika afya ya uzazi na ile ya jamii, elimu pamoja na ujasiliamali.
Mkutano huo umeongozwa na kauli mbiu isemayo “Miaka 22 ya Club za Fema Tanzania,Jukumu la ulinzi wa moto ni la kila mwana Jamii,kataa ukatili jenga maadili”