Rais wa Kenya William Ruto amelihutubia taifa usiku wa kuamkia Jumatano na kusema maandamano ya kupinga ongezeko la kodi na ushuru yalivamiwa na makundi ya wahalifu na kuapa kuwa matukio kama hayo hayatojirudia tena.
Ruto ameapa kwamba matukio ya uvamizi wa Bunge aliyoyaita “kitisho kwa usalama wa taifa”, kamwe hayatojirudia kwa gharama yoyote.” Hayo yanajiri wakati jumuiya ya kimataifa ikielezea wasiwasi wake kutokana na hali ya vurugu inayoshuhudiwa nchini humo.
Kupitia televisheni, Rais William Ruto wa Kenya ameapa kuchukua msimamo mkali dhidi ya “vurugu na machafuko” yaliyoshuhudiwa hapo jana baada ya maandamano ya kupinga mapendekezo ya serikali yake ya kupandisha kodi na ushuru kugeuka kuwa ya vurugu huku akilaani uvamizi wa Bunge :
” Cha kusikitisha zaidi, shambulio la leo dhidi ya utaratibu wa Katiba ya Kenya limesababisha watu kupoteza maisha, pia uharibifu wa mali, unajisi wa taasisi na nembo za uhuru wetu. Matukio ya leo yanaashiria mabadiliko muhimu ya jinsi tunavyoshughulikia vitisho kwa usalama wa taifa letu. Nalihakikishia taifa kuwa serikali imekusanya rasilimali zote ilizokuwa nazo ili kuhakikisha kuwa matukio ya aina hii hayatajirudia tena na kwa gharama yoyote ile.”
Rais Ruto aliwaambia waandishi habari kuwa Serikali yake itatoa jibu kamili na mwafaka wa haraka kwa matukio ya uhaini akisema maandamano hayo yalivamiwa na watu hatari.
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Kenya Adan Duale ameamuru jeshi la nchi hiyo kupelekwa mitaani na sehemu mbalimbali ya nchi kusaidia polisi kukabiliana na kile alichokiita kuwa dharura ya kiusalama.
Wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, polisi na vikosi vya usalama kujizuia na matendo ya kutumia nguvu kupita kiasi huku akitoa wito wa kufanyika maandamano ya amani.
Zaidi ya mataifa kumi ya Magharibi yameelezea wasiwasi wao mkubwa kufuatia ghasia zilizoshuhudiwa hapo jana ambapo watu watano wameripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Katika taarifa yao ya pamoja, balozi za nchi 13, zikiwemo Canada, Ujerumani, Uingereza na Marekani, zimetaja kushtushwa mno na matukio yaliyoshuhudiwa nje ya Bunge la Kenya.
Wasiwasi kama huo umetajwa pia na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ambaye ameitaka nchi hiyo kuwa na utulivu na kujiepusha na ghasia zaidi.