Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza
Juni 24, 2024 watumishi wanne ambao ni maafisa uchumi, wahasibu na maafisa uvuvi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka pamoja na Ufujaji na Ubadhilifu wa Sh. Millioni 67 kinyume na vifungu vya 28(2),(3) na 31 vya PCCA sura ya 329 na marejeo yake ya mwaka 2022.
Washtakiwa hao katika nyakati tofauti Kati ya Julai 1, 2020 hadi Juni 30 ,2021 wametenda makosa hayo wakiwa na nia ovu walitumia madaraka yao vibaya na kushindwa kuwasilisha fedha za mapato ya Serikali zaidi ya Shs. Millioni 67 kwenye akaunti ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Mapato hayo ni makusanyo mbalimbali ya fedha za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Kitendo cha kutokuwasilisha benki fedha hizo za Serikali ni kinyume na kifungu cha 50(5) ya Memoranda ya Fedha za Halmashauri za mwaka 2009, ambazo kimsingi walijipatia manufaa binafsi.
Mashauri manne dhidi ya watumishi hawa wa Serikali yamefunguliwa Juni 24, 2024 mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi Mhe. Christian Mwalimu wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, na yamesomwa mahakamani na Waendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Wakili Jovine Majura na Hilal Nikitas.
Watumishi waliofikishwa Mahakamani ni:-Hellen Mcharo ambaye ni Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mwenye case namba 17146/2024.
Medard Chenyambuga ambaye ni Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Manispaa mwenye case namba 17147/2024.
Speratus Cosmas ambaye ni Mhasibu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mwenye case namba 17148/2024.
Winning Temu ambaye ni Mhasibu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mwenye case namba 17149/2024.
Washtakiwa wote wamekana makosa yao na wawili wapo nje kwa dhamana na wawili wako rumande kwa kushindwa kukidhi vigezo vya dhamana.
Kesi hizo zitakuja tena Mahakamani Julai 4 na 18 Julai, 2024 kwa ajili ya Hoja za awali.
TAKUKURU – Mwanza Juni 25, 2024