Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Juni 24, 2024, imeamuliwa kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 11/2022 mbele ya Isiaqa Kuppa – Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Katika shauri hilo lililoendeshwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Janeth Kafuko katila Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, imemtia hatiani mshtakiwa Chema Hamisi Kalembo Mtendaji wa Mtaa wa Oysterbay, kwa kosa la ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [CAP 329 RE 2019] vikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu uchumi Paragraph 21 ya Jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Imeelezwa kuwa mshtakiwa akiwa Afisa Mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Oysterbay alitenda kosa hilo la ubadhirifu wa fedha za umma kiasi cha shilingi 12,000,000 ambazo zilikuwa ni pesa za makusanyo ya ada ya taka alizotakiwa kuziwasilisha benki na badala yake kuzitumia kwa matumizi yake biafsi.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya upande wa Jamhuri kuthibitisha kesi pasipo kuacha shaka yoyote.
Mahakama imemhukumu mshitakiwa kifungo cha miaka 20 gerezani bila faini.