Tunakubali rushwa ni adui wa haki? (4)
Ni miaka 17 sasa tangu Tume ya Kero ya Rushwa ilipotufahamisha mianya na sababu za kuwepo rushwa, wala rushwa na njia za kuitokomeza. Lakini kilio kikubwa cha madhara ya rushwa bado kinasikika kutoka kwa wananchi.
Katika sehemu ya tatu ya makala hii nilishauri Serikali ambayo ndiyo kiongozi na msimamizi mkuu wa kupambana na rushwa lazima ichukue hukumu kali dhidi ya watu wanaoendesha ‘dude’ la rushwa, ndipo kilio kitaisha.
Serikali lazima ‘ijitafune yeneyewe’ kwa maana ya kuwasulubu watendaji wanaotuhumiwa kula rushwa. Tuhuma zinatosha kuadhibu watuhumiwa. Kutafuta uthibitisho wa sheria ni dhahiri ni kutafuta upenyo wa kutoka ndani ya rushwa.
Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa aliahidi kupambana na rushwa wakati wakigombea wadhifa huo kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1995, na alipochaguliwa aliunda Tume ya Rushwa kushughulikia rushwa.
Kauli yake ilipokewa kwa shangwe na wananchi. Alipopewa orodha ya watuhumiwa wa rushwa, akabadili mwelekeo kwa kutumbukiza sheria kwanza ithibitishe.
Alifanya yale yale ya rais aliyemtangulia, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, sheria kwanza kabla ya hukumu. Kwa mtaji huo hatufiki popote.
Tume imesema chanzo kikuu cha rushwa nchini ni ‘uongozi zembe’ unaosababisha kuwepo kwa rushwa kabambe inayoongozwa na viongozi na watendaji wenye uamuzi kitaifa. Ndio hao leo wanatusumbua.
Kila siku wananchi wanalia kuhusu mikataba inayohalalisha mali na rasilimali za Taifa kuporwa, fedha za umma kuhamishiwa nje ya nchi kiujanjaujanja, miradi ya maendeleo kutekelezwa chini ya viwango, wananchi kunyimwa stahiki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kupata huduma bora za kijamii.
Nia siyo kuorodhesha matukio ya rushwa kwa sababu tunayafahamu. Nia ni kuitaka Serikali iongeze kasi katika kudhibiti rushwa kwa kuwakamata na kuwahukumu watuhumiwa.
Mbona msingi wa kukamata watuhumiwa ni tuhuma, vipi tuhuma isiwe kigezo cha kutoa hukumu?
Natambua na kukubali kuwa kuna haki za msingi za binadamu. Mbona binadamu huyo kavunja misingi ya binadamu? Sheria inasisitizwa itumike baada ya tuhuma kuwasilishwa, lakini mtoa haki na sheria zake kibindoni, anatuhumiwa kula rushwa! je, jawabu litapatikana?
Baadhi ya wananchi wanashauri zitungwe sheria na hukumu kali kuwabana wala rushwa. Mbona sheria zilizopo ni kali na bado rushwa ipo? Nadhani kinachotakiwa si sheria na hukumu kali. Kinachotakiwa ni uthubutu wa dhati na miiko ya uongozi.
Naikumbusha Serikali kutambua kuwa rushwa ni adui wa haki; na sheria na haki ni vitu viwili tofauti. Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere alipata kusema “Rushwa ni jambo la hatari kabisa, huwezi kununua haki. Haki hainunuliwi, thamani yake ni shilingi ngapi?”
Serikali iace purukushani, vyombo vya haki viache kupinda sheria na wananchi tuache huruma ya panya kuuma na kupulizia machungu wakati tunataka kuondoa rushwa. Daima sungu la udele linauma sana lakini mtoto lazima azaliwe, vinginevyo mzazi na mtoto watakufa.
Namalizia makala yangu hii kwa kukariri maneno ya Adili. Kila mara baada ya kuyapiga manyani (ndugu zake) aliyanasihi akilia:
Nala sumu ndugu zangu, Msambe naona tamu,
Takatifu kubwa kwangu, kuadhibu yangu damu,
Sina raha ndugu zangu, Neno hili kwangu gumu.
(Kitabu: Adili na Nduguze. Mwandishi: Shaaban Robert)