Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato

KATIKA kile kinachoonekana ni kuitafsiri kwa vitendo falsafa ya Polisi Jamii na Ulinzi shirikishi,Jeshi la polisi wilayani Chato mkoani Geita limefanya usafi na kutoa zawadi mbalimbali kwa baadhi wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali ya wilaya hiyo.

Mkuu wa polisi wilaya ya Chato,SSP. Fredy Mpandula, ameliambia Jamhuri Digital kuwa matendo hayo ni kuendelea kuisogeza karibu jamii katika ushiriki wa masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kupeana taarifa za uharifu na waharifu, kwa lengo la kuhakikisha jamii inaishi salama na kuendelea kutimiza wajibu wake katika kujiletea maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.

“Tumetumia fursa hii kuja hapa hospitali ya wilaya kufanya usafi na kutoa chochote kwa wagonjwa waliolazwa hapa,tunatambua kuwa sisi ni sehemu ya Jamii kwahiyo ni muhimu kushiriki kwa karibu katika masuala ya kijamii ikiwemo kuwasalimia wagonjwa na kuendelea kudumisha mahusiano”

“Mambo haya tunatekeleza ikiwa ni wiki ya utumishi wa umma nchini,na sisi kama jeshi la polisi wilaya ya Chato tunaendelea kuwahakikishia wananchi kuwa tuko pamoja nao katika suala zima la ulinzi na usalama wa mali zao” amesema Mpandula.

Hata hivyo ametoa wito kwa jamii kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya kiharifu kabla na baada ya kutokea ili kuimalisha amani na usalama wa taifa kwa ujumla.

Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Chato,Dkt. Madili Sakumi,amepongeza mkakati wa jeshi la polisi kushiriki katika suala la usafi wa hospitali hiyo sambamba na kusaidia wahitaji Sukari,Sabuni na juisi kwa wagonjwa waliopo wodini.

Amezitaka taasisi zingine kuiga mfano huo kwa sababu uhitaji wa huduma na faraja kwa wagonjwa ni jambo muhimu sana katika kurejesha afya kwa wahusika.

Baadhi ya wagonjwa waliopokea msaada huo mbali na kulipongeza jeshi la polisi wameahidi kushirikiana na taasisi zote za umma katika kuhakikisha ulinzi na usalama unaimalika nchini.