Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Kaimu Katibu Tawala ,Mkoa wa Pwani ,Shangwe Twamala amesisitiza ulazima wa Taasisi za Umma kutumia mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa Umma “NeST” ambao unasimamiwa na mamlaka ya udhibiti wa ununuzi wa Umma(PPRA).

Hayo aliyasema wakati akifungua mafunzo ya siku tano juu ya Mfumo wa NeST kanda ya Pwani yaliyofanyaki Wilayani Bagamoyo.

Twamala alieleza kwamba matumizi ya mfumo huu ni maagizo ya Serikali hivyo mahitaji yote katika ofisi za Umma lazima yanunulliwe kwa kutumia mfumo huo.

Alisema, waraka namba 2. wa Hazina unaotaka taasisi zote za Umma kufanya manunuzi kupitia mfumo wa NeST.

“Pamoja na kuwa matumizi ya mfumo ni agizo la Serikali pia ni matakwa ya sheria yanayobainishwa katika sheria mpya ya ununuzi sheria no 10 ya mwaka 2023”

Twamala alielezea, mfumo huo ni rahisi na rafiki kuutumia . Pia umesaidia kuondoa tabia za urasimu iliyokuwa ikijitokeza kipindi cha mfumo wa Zamani pia umeongeza ushirikishawaji wa watumiaji kwa kuwa wanaomba mahitaji kwa kutumia mfumo.

“Mfumo huu wa NeST umeleta uwazi zaidi ukilinganishwa na ule wa awali wa TANePS ambao ulikuwa na changamoto mbalimbali ambapo ushirikishwaji ulikuwa mdogo sana na uliruhusu baadhi ya taratibu za ununuzi kufanyika nje ya Mfumo.

Katika hatua nyingine Twamala aliishauri PPRA kuweka mikakati ya kuhakikisha wanapata washiriki wengi katika mafunzo ili mfumo huu ufahamike na watumiaji wengi .

Aliipongeza PPRA kwa kuendelea kuwa wabunifu kwa kutumia wataalamu mbalimbli wa TEHAMA na sheria kuhakikisha ununuzi wa mahitaji ya Umma unafanyika kwa uwazi ili kuongeza tija katika kupata mahitaji kwa haraka na yenye thamani halisi ya fedha.

Mafunzo hayo yamewashirikisha watumiaji wa mfumo kutoka T0aasisi mbalimbali za Umma kutoka mkoani Tanga, Morogoro na Pwani.

Mwisho