Na Mussa Juma ,JamhuriMedia,Dodoma
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Simiyu, Minza Mgika ameipongeza Kampuni ya Utalii ya Mwiba Holding Ltd ambayo imewekeza wilayani Meatu mkoa wa Simiyu ,kwa kuendelea kutoa chakula cha bure kwa wanafunzi 850 wa shule ya msingi Makao.
Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd, kupitia taasisi yake ya Friedkin Conservation Fund(FCF) ilizindua mradi wa chakula cha mchana bure katika shule ya msingi Makao mwezi June mwaka Jana ikiwa ni sehemu tu ya miradi ya jamii inayofadhiliwa na Taasisi hiyo.
Kampuni hiyo inatoa kila mwezi kiasi sh 11.5 milioni kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wa shule hiyo,pia imejenga jiko la kisasa kwa ajili ya shule hiyo lililogharimu kiasi cha sh 37.4 milioni na mradi wa uvunaji Maji ya mvua uliogharimu sh 30.8 milioni.
Akichangia hutuba ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mbunge Minza Mjika(CCM) alisema chakula cha bure ambacho kinatolewa katika shule hiyo kimeondoa utoro na shule inategemea kiwango cha ufulu kuongezeka.
Alisema Kampuni hiyo ya Mwiba pia ametoa baiskeli 200 zenye thamani ya sh millioni 40 kwa kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Paji iliyopo pia wilayani Meatu mkoa wa Simiyu.
“Tunaipongeza Kampuni hii pia imejitahidi kujenga Nyumba za walimu na wahudumu wa afya na imekamilisha ujenzi wa madarasa”alisema
Mbunge huyo alipongeza pia Waziri wa Maliasili na Utalii Angella Kairuki na Naibu Waziri na watendaji wengine wa Wizara kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitoa kwa wananchi wa wilaya ya Meatu katika sekta ya Utalii na uhifadhi.
Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd inafanya shughuli za Utalii na uhifadhi katika eneo la ranchi ya wanyamapori ya Mwiba na Pori la Akiba Maswa.
Meneja miradi wa Kampuni Aurelia Mtui alisema Kampuni hiyo imetenga dola 793,000 ambazo ni zaidi ya Sh 2 bilioni ili kuchangia shughuli za maendeleo ya jamii.
Mtui alisema ,fedha hizo zilizotengwa mwaka 2024 zimeongezeka kwani mwaka 2023 zilikuwa zimetengwa na kutumika kiasi cha dola 525,000 ambazo ambazo ni zaidi ya Tsh 1.2 bilioni.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Meatu,Anthony Philipo pia amekuwa alipongeza mchango wa Mwiba Holdings Ltd kupitia Friedkin Conservation Fund, katika wilaya hiyo, alisema ni mkubwa katika kusaidia jamii,chakula mashuleni,ujenzi wa madarasa ,nyumba za walimu na madaktari na vifaa na mafunzo jinsi ya kudhibiti migogoro kati ya binadamu na wanyamapori hasa tembo.