Katika mitandao ya kijamii na makundi sogozi, zinasambaa taarifa potofu kuhusu uhalisia wa Gawio la Shilingi Bilioni 153.9 lililotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa Serikali kwa mujibu wa Sheria kwa mwaka 2024. Kufuatia taarifa hizo potofu, Menejimenti ya TPA inapenda kutoa ufafanuzi wa suala hilo kama ifuatavyo:-

Kwanza, Taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii na makundi sogozi si taarifa sahihi, ni potofu na imetolewa kwa nia ovu ya kuupotosha Umma, kuichafua TPA na kurudisha nyuma juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo kwenye Sekta ya Bandari Nchini.

Pili, Taarifa sahihi ni kwamba, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kutekeleza matakwa ya Sheria kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kuwasilisha Serikalini Gawio la Asilimia 15 ya Mapato Ghafi kwa mwaka wa fedha husika, imetekeleza takwa hilo la Kisheria kwa kuwasilisha Gawio la Shilingi 153,917,950,278.75 /= (Bilioni mia moja hamsini na tatu, milioni mia tisa kumi na saba, laki tisa hamsini elfu mia mbili sabini na nane na senti sabini na tano) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Tatu, Gawio hili la Tsh. 153.9b imetokana na mapato ghafi ya Robo tatu kati ya nne za mwaka wa fedha 2023/2024 ambayo ni miezi 9, kuanzia Julai 2023 hadi Machi 2024.Makusanyo ya mapato kwa kipindi hicho ilikuwa TZS 1,038,019,808,000/= (Trilioni moja, milioni, bilioni thelathini na nane, milioni kumi na tisa, laki nane na elfu nane. Kwa mapato hayo TPA kwa mujibu wa Sheria ilipaswa kutoa Gawio la TZS 155,702,971,200/= Bilioni mia hamsini na tano, milioni mia saba na mbili, laki tisa sabini na moja elfu na mia mbili, pesa iliyobalki ambayo ni 1,785,020,921.25/= Bilioni moja, milioni mia saba themanini na tano, elfu ishirini mia tisa ishirini na moja na senti mbili tano, itawasilishwa kabla ya kufungwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwa ni mapato ghafi ya robo ya nne kwa mwaka 2023/2024.

Nne, Ufafanuzi kuhusu gawio la TZS Bilioni 480 lililowasilishwa serikalini na TPA kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ni kama ifuatavyo:
Kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019, Gawio la mchango wa asilimia 15 ya mapato ghafi lililotolewa na TPA kwa serikali ni TZS Bilioni 141.3 ambalo lilikuwa ni sawa na asilimia 15 ya mapato ghafi kwa mwaka huo ya TZS Bilioni 938 yaliyokusanywa. Fedha nyingine zilizotolewa zilikuwa ni bakaa ya Gawio la miaka mitano ya nyuma kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2017/2018 yenye jumla ya TZS Bilioni 338.7 Bilioni hivyo kufanya jumla ya fedha yote iliyowasilishwa serikalini kama gawio kuwa TZS Bilioni 480 kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Hivyo Gawio la TZS Bilioni 480 lililotolewa mwaka wa fedha 2018/2019 halikuwa gawio lililotokana na asilimia 15 ya mapato ya mwaka mmoja wa fedha 2018/2019 kama ilivyosemwa katika taarifa hiyo.

    Tano, Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inapenda kuujulisha umma kwamba, itaendelea kutimiza Wajibu na Majukumu yake kikamilifu kwa mujibu wa Sheria, ikiwa ni Pamoja na kutoa Gawio Serikali kwa mujibu wa Sheria kila mwaka wa fedha husika unapofikia mwisho.