Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimesema kuwa wananchi bado wanahitaji Katiba Mpya ambayo ni mustakabari wa Nchi.
Kutokana na hilo, TLS imeendelea kutimiza wajibu wake kwa umma kwa mujibu wa sheria ambapo imeendesha miadala kwa wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini juu ya ‘Mchakato wa Upatikanaji wa Katiba Mpya’.
Akizungumza wakati akifungua Mjadala huo, Mkurugenzi wa Mtendaji wa TLS, Mariam Othuman amesema wameamua kuandaa mjadala na kundi hilo la vijana ambalo ni muhimu na wamekuwa wakifanya hivyo kwa makundi mbalimbali.
“Kwa kuangalia majukumu tuliyonayo pamoja na Mchakato wa Katiba unaoendelea tukaona kuna umuhimu wa kuanzia mijadala mbalimbali ya kuongelea masuala ya mchakato wa Katiba Mpya.
“Hivyo tukaona ni vyema kupitia kundi Maalum ambapo kundi la vijana ni mojawapo na tukiangalia sensa ya mwaka 2022 inasema asilimia 34.5 ya Watanzania ni vijana. Kwahiyo tukaona hili ni kundi muhimu sana kuwasikiliza na kupokea maoni yenu juu ya mchakato wa Katiba Mpya. Hivyo tunaamini mtatoa maoni yenu kwasababu nyie ndo chachu ya maendeleo katika Taifa. Tunawatia moyo yote ambayo tutajadili hapa tutayachukua na kuyafanyia kazi ili tuweze kuyafikisha katika mamlaka husika,” amesema Mariam.
Ofisa Miradi TLS, Victor Mbuligwe amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ina mapungufu na ndio maana ulianzishwa mchakato wa kupata Katiba Mpya ambao mwaka 2014 ulikwama.
“Lakini sasa hivi tunaona serikali ina nia ya dhati kuufufua huo mchakato kwahiyo sisi tumeamua kuanza kuyakusanya haya Makundi tofauti ili kupata maoni yao kitu gani ambacho wanafikiri kiwepo kwenye hiyo katika mpya wanayoitarajia.
“Mstakabari wa Nchi ni Katiba na Katiba ni Sheria mama, na Sheria ambayo inatengenezwa na wananchi wenyewe. Hivyo bado sisi tunahitaji Katiba Mpya na inahitajika na wananchi na kwa kauli ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwahi kusema wananchi wanahitaji Katiba yao,” amesema Mbuligwe.
Naye Thomas Alfred ambaye ni wanafunzi wa Chuo cha Sheria amesema amesema mijadala hiyo ni muhimu kwa wakati huu ambao kilio kikubwa ni kupatikana kwa Katiba Mpya.
“Ukiangalia maendeleo ya sasa katika Nchi yetu ni kweli tunahitaji Katiba Mpya. Kwa mfano kuna vifungu ambavyo vipo kwenye Katiba vinasema kama kuna Sheria yoyote inakinzana na vifungu vya Katiba basi sheria hiyo ni batili, na tunaona kuna Sheria ambazo vifungu vyake vinapingana na Katiba lakini zinaendelea,” amesema Thomas.