Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaji Abubakari Kunenge amemuapisha Petro Magoti (Juni 14) kuwa mkuu mpya wa Wilaya ya Kisarawe na kumuagiza kuhakikisha anaweka kipaumbele katika suala zima la ulinzi na usalama katika wilaya hiyo.
Katika halfa hiyo ya uapisho imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali viongozi wa chama,wakurugenzi,waku wa Wilaya,wakuu wa idara pamoja na wageni wengine .
Mara baada ya kuapishwa ,Magoti alitoa shukrani kwa Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumchagua katika nafasi hiyo.
Magoti aliahidi kushirikiana bega kwa bega na viongozi wa wilaya ya Kisarawe na Mkoa wa Pwani kwa lengo la kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi.
“Nashukuru kwa dhati kwa Rais kuweza kunichagua katika nafasi hii na mm nitakuwa mstari wa mbele katika kusaidia na viongozi wenzangu katika kuwatumikia wananchi wa Wilaya ya Kisarawe “, alifafanua Magoti.
Vilevile Magoti alieleza ,ataonyesha taswira nzuri kwenye uwajibikaji katika uongozi wake na kwamba atayatekeleza yale yote ambayo ameagizwa na Rais kuyatekeleza katika sekta mbali mbali.
“Nchi hii ya Tanzania ina watu wengi sana ambao ni wasomi na wengine wana uwezo mkubwa lakini mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweza kumpendeza na kuamua kunichagua katika nafasi hii na mm namwomba Mungu anijalie niwe mtiifu katika kazi hii,”alieleza Magoti.
Kadhalika Mkuu huyo amemwakikishia Mkuu wa Mkoa wa Pwani kumpa ushirikiano wa kutosha yeye pamoja na wasaidizi wake.
Magoti alieleza, katika kutekeleza majukumu yake atahakikisha anafanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia misingi ya kuwa na mshikamano na utiifu.
“Mimi nimefanya kazi Ikulu na Rais wetu kwa kweli anachapa kazi kweli usiku na mchana maana halali kwa hivyo na sisi viongozi tunapaswa kuiga mfano wake katika kutimiza wajibu wetu,”alieleza Magoti.
Nae Kunenge ametaka wakuu wa wilaya kuendelea kusikiliza kero na changamoto mbalimbali za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.