Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao kuhabarisha na kuelimisha wananchi kuendelea kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji na maelekezo ya Tume kuhusu zoezi la uboreshaji wa daftari la mpiga kura.
Wito huo umetolewa leo Juni 13, 2023 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa Tume hiyo na waandishi wa habari.
Amesema Tume imeanza mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo utazinduliwa rasmi Julai 01, 2024 mkoani Kigoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Amesema wakati wa zoezi hilo, Tume imeweka utaratibu kwa watu wenye ulemavu, wazee, wagonjwa, wajawazito na wakina mama wenye watoto wachanga watakaokwenda nao vituoni kupewa fursa ya kuhudumiwa bila kupanga foleni.
“Tunaomba waandishi wa habari kupitia kalamu zenu muwafahamishe wananchi wote waliopo kwenye makundi tajwa kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha au kuboresha taarifa zao vituoni kwa kuwa utaratibu mzuri wa kuwahudumia umewekwa.
“Tume inaamini kuwa uwepo wa uwakilishi huu mpana wa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kwenye mkutano huu utasaidia katika kuongeza wigo wa kuwafikia wadau wa Uchaguzi na wananchi kwa ujumla haswa katika kipindi hiki cha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” amesema.
Ameongeza kuwa Tume imejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu uboreshaji huo, na njia mbalimbali za kutoa elimu ya mpiga kura zitatumika ili kuhakikisha kwamba wadau wote wanapata fursa ya kuelimika na kuelewa mambo yote ya msingi kuhusu uboreshaji huo ili wajitokeze kwa wingi kushiriki kwenye zoezi hilo.
Jaji Mwambegele ameongeza kuwa, Tume itaendelea kuweka milango wazi kwaajili ya kutoa taarifa za mara kwa mara na katika kipindi chote cha uboreshaji wa Daftari itakuwa na kituo cha huduma kwa wateja, ambapo wadau wa Uchaguzi na wananchi kwa ujumla wanaweza kupiga simu na kujibiwa maswali mbalimbali yanayohusiana na uboreshaji wa Daftari.
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima amesema INEC kwa sasa inaendelea na mchakato wa kupitia maombi ya vibali vya elimu ya mpiga kura pamoja na uangalizi wa zoezi la uboreshaji wa daftari la mpiga kura huku tume hiyo ikitegemewa kutoa orodha ya taasisi na asasi hizo zilizopitishwa kushiriki katika zoezi hilo kuanzia mwishoni mwa mwezi huu.
Kuhusu masuala ya usalama wa taarifa na matumizi ya teknolojia katika zoezi hilo, Mkurugenzi wa Daftari la Mpiga Kura na Tehama, Stanslaus Mwita amesema Tume imesha nunua BVR mashine 6000 kwa ajili ya kutumia katika vituo zaidi ya 40,000 kwa awamu 13 huku akibainisha maboresho mengine katika programu na namna ya uendeshaji zoezi hilo yalivyo boreshwa.