Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Darbea Salaam
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewaasa wahariri wa vyombo vya habari kuwahabarisha na kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa Tume na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo tarehe 12 Juni, 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesisitiza juu ya umuhimu wa vyombo vya habari na nafasi yao katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.
Mkutano huo ambao ni mwendelezo wa vikao vya wadau vilivyoanza tarehe 07 Juni, 2024 ulikuwa na lengo la kuwapa wadau hao wa uchaguzi taarifa mbalimbali za maandalizi kwa ajili ya kuanza rasmi kwa zoezi la uboreshaji wa daftari.
“Tume inatarajia kupata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwenu, kwa kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu zoezi lililopo mbele yetu la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwahamasisha wananchi wenye sifa ya kujiandikisha kuwa wapiga kura, wajitokeze kwa wingi kwa tarehe ambazo Tume imeziweka kwa kila kituo,” amesema Jaji Mwambegele.
Amewashukuru wahariri hao kwa kuwa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitoa fursa kwa Tume kutumia vipindi vya redio na televisheni kutoa elimu ya mpiga kura ikiwa ni pamoja na kutoa fursa ya kuchapisha habari na makala kwenye magazeti za kutoa elimu na kufafanua hoja mbalimbali zinazotolewa na wadau wa uchaguzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Bw. Kailima, R. K ameviasa vyombo vya habari kuelimisha wananchi kuzingatia sheria, kanuni, miongozo, taratibu na maelekezo yanayohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura badala ya kulalamika.
“Kupitia vyombo vya habari tuwashauri wote watakaodhani kuna changamoto kutumia njia zilizopo kwenye sheria, kanuni, miongozo, taratibu na maelekezo yanayohusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura badala ya kuanza kulalamika,” amesema.