RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini kujenga jamii na taifa kiroho ikiwa ni njia ya kukabili kuporomoka kwa maadili hasa kwenye familia.
Rais Samia alisema hayo jana wilayani Sumbawanga kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa kwenye ibada ya kusimikwa kazini Mchungaji Imani Kibona kuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Ziwa Tanganyika.
Askofu Kibona anachukua nafasi ya Askofu Ambele Mwaipopo ambaye amestaafu. Katika hotuba hiyo, Rais Samia alisema familia nyingi zina changamoto mbalimbali kutokana na sababu tofauti ikiwamo jamii kutojengeka kiroho.
Alisema katika Ripoti ya Utafiti ya mwaka 2022 ya ufuatiliaji wa kaya ilionesha
kuwa kuanzia mwaka 2020 hadi 2022 ilionesha kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania wenye umri wa kuolewa na kuoa hawajaingia kwenye ndoa.
Rais Samia aliongeza kuwa idadi hiyo inawakilishwa na wastani wa asilimia 61 kwa upande wa mijini huku eneo la vijijini likiwakilishwa na asilimia 55.
Alisema waliobahatika kuingia kwenye ndoa pia kuna hali mbaya kwani wanakabiliwa na migogoro. Alitoa mfano kuwa katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2023, kuna mashauri ya migogoro ya ndoa 39,579.
Alisema katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2023/2024 , kuna mashauri ya migogoro ya ndoa yapatayo 28,773 hali aliyosema inachangiwa na wanandoa kutokuwa karibu na Mwenyezi Mungu.
Katika hatua nyingine, alisema kutokana na watu kumsahau Mungu wamekosa baraka zake na kusababisha kuwa na roho zisizo za kibinadamu hali iliyosababisha kuongezeka kwa vitendo vya kikatili dhidi ya binadamu.
Aliongeza kuwa takwimu za Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa mwaka 2023 kulikuwa na matukio ya udhalilishaji 30,569 huku mwaka 2024 yakiripotiwa matukio ya udhalilishaji 29,073 hali inayoonesha kuwa mwaka huu kutakuwa na ongezeko la matukio hayo.
Kutokana na hali hiyo, Rais Samia aliwataka wazazi pamoja na viongozi wa dini kuipa familia kipaumbele na
umuhimu mkubwa kuhakikisha changamoto hizo zinakwisha.
Kwa upande wake, askofu Kibona aliyeingizwa kazini, alieleza kusikitishwa namigogoro inayoendelea katika kanisa. Alisema kwa hali ilivyo, lazima dayosisi ijitokeze mstari wa mbele ikemee na kupiga vita migogoro kwani inarudisha nyuma maendeleo nchini.
“Nidhamu kwa Dayosisi ya Ziwa Tanganyika ni muhimu, na kuwakemea wale wote wanaovuruga amani ya dayosisi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.
Viongozi tuache kusambaza uzushi na matusi katika mitandao ya kijamii,” alisema askofu Kibona. Alisema mitandao ya kijamii inapaswa kutumika kusambaza neno la Mungu linalobeba upendo, matumaini na amani duniani badala ya kutumika kuchochea vurugu na kuharibu amani ya nchi.
Askofu Kibona aliomba serikali kuwachukulia hatua wote wanaotumia mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari kuleta uchochezi, vurugu pamoja na kuwatukana viongozi wa dini na kanisa. Alisema hatua hiyo italeta heshina na nidhamu kwa taasisi hizo.
“Yeyote anayemtafuta mtu amfanyie ubaya, ajue kuwa hata yeye mwenyewe anatafutwa mbinguni,” alisema askofu Kibona.
Askofu huyo alitangaza msamaha kwa waumini wa dayosisi hiyo waliojitenga na
kanisa na kufanya ibada nje ya kanisa kwa kuwataka warudi kanisani bila masharti yeoyote. Katika hatua nyingine, alimshukuru Rais Samia kwa kuwekeza katika miundombinu hali iliyomfanya kusafiri kwa njia ya barabara nchi nzima katika harakati za kichungaji.
Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa alipongeza juhudi za serikali zilizoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kujenga taifa lisilo na ukabila, udini, itikadi na ukanda akisema imechangia Tanzania kuwa taifa la amani na utulivu.
Dk Malalusa alisema hali hiyo imewafanya viongozi wa dini mbalimbali kuhudhuria na kuingia katika nyumba za ibada ambazo si za imani yao katika matukio mbalimbali. Ibada hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Rukwa, Shehe Mohamed Adam aliyemwakilisha Shehe wa Mkoa wa Rukwa, Rashid Akilimali.