Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Chama Cha Alliance for Democrac Change (ADC) Taifa, Doyo Hassan Doyo ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Uenyekiti Taifa baada ya Mwenyekiti wa sasa Hamad Rashid Mohamed kumaliza muda wake kikatiba.
Akitangaza nia yake leo Juni 6, 2024 jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, amesema ameona kuwa anaamimi ana uwezo wa kukitumikia Chama hicho katika kutekeleza matakwa ya Katiba.
“Kutokana na uzoefu wa miaka 10 nilioupata kutoka kwa Mwenyekiti aliiyemaliza muda wake naahidi kuyaendeleza mazuri yote hususani kuilinda Katiba ya chama.
“Mwenyekiti Hamad ametufunza jambo katika chama kwani ameonyesha kufuata matakwa ya Katiba kwa kuachia ngazi baada ya kumaliza muda wake na kuwapa funzo vijana wa chama hicho na wanasiasa wengine nchini wanaong’ang’ania madaraka,” amesema Doyo.
Amebainisha kuwa, Juni 11 mwaka huu atachukua fomu rasmi kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo na kuwaomba wanachama wenzake ndani ya chama itakapofika Juni 27 mwaka huku wamchague Ili aweze kufanya yote aliyokusudia na Chama kiweze kufikia viwango vya juu.
Ameongeza kuwa, endapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo atakisaidia Chama kusukuma ajenda za upatikanaji wa ajira, elimu Bora,na kupata wabunge wawakilishi watakaowakilisha wananchi katikà changamoto zao bungeni.
Naye Mwenyekiti wa Vijana Taifa Ibrahimu Pogora amempongeza Doyo kwa kutangaza nia yake na kuahidi kushirikiana naye katikà harakati zote za uchaguzi, kupata wadhamini Bara na visiwani.
Amewataka wanachama wa Chama hicho kutambua kuwa wanadhamana na mtia Nia wa nafasi hiyo kwa kuwa Doyo si mwanachama wa kuletwa bali ni mwanzilishi wa Chama hicho
Wakati huo huo, Scola Kahana aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Kibaha Mjini mwaka 2020 kupitia Chama hicho ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa Ili aweze kushirikiana na Mwenyekiti Taifa kukinoa Chama hicho na kukiwezesha kuwa Chama Cha mfano.