Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Siku moja ukipata nafasi ya kukaa na mjukuu wako kupiga nae stori ya mashujaa wa soka la Tanzania basi usiache kumuelezea kuhusu John Raphael Bocco, ambaye jana amestaafu rasmi kuutumikia mpira kama mchezaji kwenye nafasi yake ya ushambuliaji aliyokuwa bora mara zote.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Bocco ameandika ujumbe mfupi wa kuwaaga na kuwashukuru klabu ya Simba, wanachama na mashabiki waliomuamini kwa muda mrefu na kumpa heshima kubwa iliyoenda mpaka timu ya taifa ya Tanzania, kama ingekuwa ni ufundi wa kutengeneza muziki basi Bocco ni S2kizzy wa Boli.
Wakati Sauti Sol anamuomba Nerea asitoe mimba yake nyie hamkumuelewa kabisa, Alikuwa anajua kuwa matumbo ya hawa mama zetu yamebeba siri nzito, na nina uhakika hata ile Agosti 5, 1989, katika hospitali ya Taifa Muhimbi wakati mama Bocco anajifungua hakujua kama ameleta shujaa duniani, walishangilia na kumshukuru Mungu kwamba mwanachama mpya ameongezeka kwenye familia tena dume la mbegu, kwahiyo dada unayesoma makala hii usiende kutoa hiyo mimba, na wewe mwamba uliyekataa mimba kimbia fasta kaombe radhi na uanze kulea, usije ukaishia kutrend baadae kumlilia mtoto wako mwenyewe mitandaoni .
Najua watoto wa elfu mbili wamemuona John Bocco dakika za Pascal Kabombe, hawaijui kabisa historia yake na ndio maana nikaona ipo haja ya kuandaa makala yake ili waelewe kwanini aliitwa Adebayor.
Bocco aliungana na Paulo na Sila kwenye maombi akiwa na timu ya mtaani kwao ya Kijitonyama FC, mpaka mwaka 2008 milango ya gereza ilipofunguka akapata nafasi ya kujiunga na Azam FC aliyofanikiwa kuipandisha ligi kuu ya Vodacom akiwa na mshkaji wake Sure Boy.
Mwaka 2009 aliitwa kwa mara ya kwanza kuichezea timu ya taifa na akaendelea kuwa sehemu ya kikosi mara kwa mara katika michuano ya kufuzu kushiriki kombe la dunia.
kwa sababu Ice Cream ni tamu sana zilimnogea Bocco akadumu Azam FC kwa miaka 10 mpaka mnyama alipovamia kiwanda mwezi juni, 2017, na kumpa kandarasi ya miaka miwili, ilipotamatika wakamuongezea tena mpaka kustaafu kwake, akiwa Nahodha wa Simba sc..
Akiwa Simba kama mchezaji kiongozi, Bocco ametwaa taji la ligi kuu misimu minne mfululizo na kufika robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika zaidi ya mara nne.
Mpaka Anastaafu kucheza soka, Bocco ndiye kinara wa mabao tangu kuanzishwa kwa ligi kuu ya Tanzania akiwa amefunga magoli zaidi ya 120.
Nimeona comment za mashabiki na wadau wa soka wakiwataka Simba kumuaga Bocco kwa heshima, nikajiuliza hivi hili kweli linahitaji D Mbili, mwisho wa siku nimeamua kuwapa Simba muda labda wamevurugwa na kukosa ubingwa wakiwa nafasi ya tatu, naamini wakitulia watafanya jambo kwa ajili yako ‘GOAT OF TANZANIA’…
Kuna msemo unasema ‘Once a Lion, you Always a Lion’, Bocco kwa sasa ni kocha wa timu ya vijana ya Simba, anatengeneza warithi wake na timu ya taifa iliyo bora.
Captain Bocco tusamehe sana kwa kutokuwa na shukrani kila ulipopitia nyakati mbaya kazini, najua kifua chako kimebeba maumivu ya kutukanwa, kubezwa na watanzania wenzako, we tusamehe tu kaka, mwisho naomba nikunong’oneze kuwa jahazi uliloliacha linazama huku, kutokana na uzoefu wako kama kuna la kushauri au kusaidia basi usiache tafadhali.
Tunakutakia kila la kheri Captain Fantastic katika majukumu yako mapya, Tutamiss vingi kutoka kwako, video zako tunazo tutaangalia hata Jangwani tukiwa na Mzize.