Mara nyingi ubingwa wa mashindano ya soka ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, umekuwa ukibebwa na Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya jijini na Dar es Salaam Young Africans (Yanga), yenye makao yake mitaa ya Jangwani na Twiga, kana kwamba timu nyingine hazina wachezaji mahiri wenye uwezo wa kushinda.

Watanzania wengi wangependa kuona na kusikia timu nyingine nazo zinajikakamua msimu huu na kufikia hatua ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo. Ubingwa wa ligi hiyo ukichukuliwa na timu yoyote nyingine, utatoa changamoto kwa timu nyingine ndogo kuongeza juhudi katika ushindani wa soka nchini. Si kwamba Simba na Yanga hazistahili au hazina haki ya kutwaa ubingwa katika mashindano hayo, la hasha, ila ubingwa ukichukuliwa na timu nyingine utazipa morali zinazodhani kuwa hazina uwezo wa kushinda.


Muda uliobaki katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo, unatosha kuzipaisha timu nyingine zilizo nyumba ya Yanga, Azam na Simba na kuziwezesha kuibuka washindi.

 

Cha msingi zaidi ni viongozi wa timu husika kuimarisha matayarisho na wachezaji wenyewe kujiamini, na kujituma zaidi dimbani ili kufikia mafanikio hayo.