Na Stella Aron,JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kufuatia marekebisho ya Katiba mwaka 1995, Serikali iliianzisha Sekretarieti ya Maadili chini ya Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977. Sekretarieti ilianza kazi zake rasmi Julai, mwaka 1996 ili kuziba pengo lililoachwa wazi na iliyokuwa Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi Na. 6 ya 1973 (The Committee for the Enforcement of the Leadership Code Act No.6 of 1973) iliyoundwa ili kudhibiti Maadili ya Viongozi ikiwa ni pamoja na kupokea na kuchunguza malalamiko ya ukiukwaji wa Miiko ya Uongozi.
Kamati hii ilifutwa mwaka 1992 baada ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa na Uchumi Huria nchini Tanzania. Viongozi kama raia wengine, wakawa na uhuru kufanya shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato. Hakukuwa na utaratibu au chombo cha kushughulikia Maadili ya Viongozi, hivyo maadili yalianza kuporomoka kwa kasi kiasi wananchi kukosa imani na Serikali kwa ujumla. Hapo ndio ilipokuja wazo la kutunga Sheria ambayo itasimamia maadili ya Viongozi wa Umma kuendana na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jukumu kuu la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kuchunguza tabia na mwenendo wa Kiongozi wa Umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya Sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo.
Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na.13 ya mwaka 1995, lengo la Sektretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kukuza na kusimamia viwango vya maadili ili kuongeza imani ya wananchi kuhusu uadilifu wa Viongozi wa Umma na katika utaratibu mzima wa kutoa maamuzi ya Serikali na katika sekta ya umma kwa ujumla.
Katika kuhakikisha kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inafikisha elimu, imekutana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), jijini Dar es Salaam na kuwajengea uwezo na namna ilivyopata mafanikio katika kipindi cha miaka mitatu ya chini ya kiongzi jemedali Rais Samia Suluhu Hassan.
Sivangilwa Mwangesi ni Kamishna wa Maadili Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi kuna umuhimu mkubwa wahariri kuwa na uelewa kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na 13 ya mwaka 1995 pamoja na mafanikio ya miaka mitano.
Akifungua mkutano huo, Jaji Mwangesi anasema kuwa vyombo vya Habari ni nguzo muhimu katika ukuzaji wa maadili kwani vinaongeza ushiriki wa wananchi katika kudumisha maadili nchini.
“Upo umuhimu wa kushirikiana na Taasisi Simamizi katika kuibua changamoto mbalimbali za uzingatiaji wa maadili na kushauri mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo.Vyombo vya Habari vinaweza vikawa na makala au vipindi maalum vinavyohimiza na kuhamasisha masuala ya maadili katika sekta ya umma na jamii kwa ujumla, ” anasema.
Anasema kuwa wahariri wanatakiwa kutumia kalamu zao kuandika umuhimu wa maadili kwa viongozi wa umma ili kusaidia kukuza uadilifu wao katika utendaji wa kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.
“Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma peke yake haiwezi kutoa elimu ya uadilifu bila msaada wa wadau wengine mkiwemo nyie wahariri wa vyombo vya habari tunawategemea sana” anasema Jaji Mwangesi.
Jaji (Mst) Mwangesi anawasisitiza wahariri kuandika makala za kichambuzi, kufanya mahojiano na wataalamu wa masuala ya maadili pamoja na wananchi, kufanya uchunguzi wa kina na kuandika ripoti za kuchambua tabia na maadili ya viongozi kwa kina.
“Katika mkutano wenu mkoani Dodoma nilimsikia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari Nape Nnauye akisema nanukuu “Wahariri na waandishi wa vyombo vya habari kwa sasa wanaandika habari bila woga wala hofu kutokana na Juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuvifanya vyombo vya habari kuwa huru,” mwisho wa kunukuu. Jamhuri toleo la 7 – 14 Mei, 2024.” anasema.
Anawashauri waandishi wa habari kuendelea kutoa habari zinazohusu miendendo ya Viongozi wa Umma.
“Nafahamu kuwa vyombo vya habari vinaweza kutumia njia mbalimbali kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu hali ya uadilifu na uwajibikaji kwa Viongozi wa Umma nchini. Baadhi ya njia hizi ni vikaragosi, tahariri, makala, nk.
“Habari hizi zinawasaidia viongozi kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na 13 ya mwaka 1995. Jukwaa hili limekuwa mdau na msaada wetu mkubwa katika kukusanya taarifa muhimu na za ukweli zinazoipa nguvu jamii kujua hali ya uadilifu nchini,” anasema.
Anasema kuwa kupitia mada hizo, wahariri watapata uelewa na mwanga wa kutosha kuhusu utendaji wetu wa kazi. Uelewa huo utawasaidia kuchambua, kutoa maoni, kuibua hoja na kuchapisha habari na makala bora zaidi kuhusu maadili ya viongozi wa umma.
“Niwaombe kwa umoja wenu, kutumia ubunifu wa kalamu zenu kuandika habari nyingi zinazoeleza umuhimu wa maadili kwa Viongozi wa Umma nchini. Tuwaondoe viongozi na wananchi hofu tunapotimiza wajibu wetu kwa mujibu wa Sheria na kanuni zilizopo. Tusaidiane kukuza Uadilifu wa viongozi wetu, kwani uadilifu wa viongozi ukiongezeka utasaidia kukuza maendeleo ya taifa na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Ninaviasa vyombo vya habari vijikite katika kujenga hoja kwa kuchapisha na kutangaza habari linganifu zilizosheheni ukweli bila upendeleo wala uonevu kuhusu maadili ya viongozi wa umma nchini. Sekretarieti ya maadili ya Viongozi wa Umma peke yake haiwezi kutoa elimu ya uadilifu bila msaada wa wadau wengine mkiwemo nyie wahariri wa vyombo vya habari. Sote kwa pamoja tushirikiane kujenga uadilifu nchini kwa kutoa elimu ya maadili na kuibua changamoto zinazokwamisha uadilifu nchini.
MAFANIKIO YA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITANO
Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Mipango Bw. Omary Juma anasema kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita wastani wa uwasilishaji malalamiko kwa mwezi umeongezeka kutoka malalamiko 16 mwaka 2021/22 hadi malalamiko 18 kwa mwaka 2022/23.
“Ongezeko hilo ni sawa na asilImia 13 hali hii inaonyesha vyombo vya habari nchini vimekuwa na mchango mkubwa wa kutoa elimu na kupelekea wananchi kupata uelewa juu ukiukwaji wa maadili,.” anasema
Sekretarieti ya Maadili imezingatia zaidi katika kufikia viwango vya juu ya uzingatiaji wa maadili kwa viongozi wa umma kwa kuboresha usimamizi na ukuzaji wa maadili kwa viongozi wa umma.
Anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa wananchi na umma kwa ujumla unakuwa sehemu ya uwajibikaji katika kukuza maadili kwa viongozi, Sekretarieti inalenga katika kuimaridha ushiriki wa wananchi katika kukuza na kusimamia maadili kwa kutoa taarifa hasa katika eneo la ukiukwaji kwa viongozi
VIPAUMBELE VYA SEKRETARIETI YA MAADILI
Anasema kuwa kwa kuzingatia jukumu kuu la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo ni kufuatilia tabia na mienendo ya viongozi na watendaji ili kubaini kwa haraka nani anajihusisha na vitendo vya uvunjifu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, vipaumbele vya Taasisi vimeanishwa kupitia Mpango Mkatati wa Taasisi wa mwaka 2022/23 – 2025/26 na pia kupitia Mipango na Mikakati ya Kitaifa ikijumuisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025
Anasema kuwa miongoni mwa vigezo vinavyotumika kupima na kutathmini uadilifu wa kiongozi ni pamoja na: ujazaji kwa usahihi na urejeshaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni; kupungua kwa malalamiko dhidi ya Viongozi wa Umma katika kukiuka Sheria ya Maadili; uzingatiaji wa hati ya ahadi ya uadilifu na sheria mbalimbali za nchi kwa kutaja baadhi ya vigezo. Hali halisi katika kipindi cha miaka mitano (5) ni kama inavyoonekana hapo chini kwa kuangalia kwa kina eneo moja baada ya moja:
TAMKO LA RASILIMALI NA MADENI
Anasema kuwa hali ya urejeshaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Viongozi wa Umma kwa wakati (kila ifikapo Desemba 31 kila mwaka) katika kipindi cha miaka mitano (5) imekuwa ni ya kuridhisha. Wastani wa urejeshaji kwa wakati umekuwa zaidi ya asilimia 96 kwa mwaka ikilinganishwa na wastani wa asilima 77 katika kipindi cha miaka kumi (10) kutoka 2009/10 hadi 2019/20.
Hali hii ya urejeshaji fomu kwa wakati limetokana na juhudi za Sekretarieti kutoa elimu kuhusu Sheria ya Maadili hususan umuhimu wa kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni.
Aidha, hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha viongozi wanafuata misingi ya maadili nayo imechangia kwa kiwango kikubwa katika kuwafanya viongozi kuwajibika na Sheria ya Maadili ikiwemo urejeshaji wa Tamko kwa wakati. Mathalan, katika mwaka 2019/20, 2020/21 na 2023/24 kiwango cha viongozi kurejesha Tamko kilikuwa juu ya wastani wa miaka mitano (5) iliyopita.
Katika kuhakikisha kuwa kiwango cha urejeshaji kinafikia asilimia 100, Sekretarieti inaendelea na juhudi za kuwasiliana na mamlaka za uteuzi ili kuhakikisha Viongozi wote hasa wale wapya wanapata taarifa au elimu ya umuhimu wa kujaza tamko la awali na lile la mwisho ili kusaidia ufuatiliaji wa tabia na mienendo kwa Viongozi.
UCHAMBUZI WA MATAMKO YA RASILIMALI NA MADENI
Kwa kuzingatia kifungu cha 19 (2) (a) cha Sheria ya Maadili, Sekretarieti ina wajibu wa kupokea Matamko ya Rasilimali na Madeni. Mara baada ya kupokea matamko husika, Sekretarieti hufanya uchambuzi kwa lengo la kubaini kama kuna viashiria vya mgongano wa maslahi, kuficha mali na kujiridhisha na usahihi wa taarifa zilizotamkwa na viongozi.
Aidha,shughuli ya uchambuzi inaiwezesha Sekretarieti katika kubaini viongozi wenye rasilimali zinazotia mashaka, rushwa na matendo mengine ya ukiukwaji wa maadili na kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria mbalimbali.
Anasema kuwa hadi kufikia Juni 2023, jumla ya matamko 13,485 sawa na asilimia 87 ya matamko 15,556 yaliyopokelewa yamefanyiwa uchambuzi ikilinganishwa na matamko 7,732 mwaka 2019/20. Hii ni sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 100 ya matamko yaliyochambuliwa ikilinganishwa na miaka mitano nyuma.
Katika kipindi husika kumekuwepo na kupungua kwa matamko yaliyokutwa na dosari kwa mwaka kwa wastani. Katika mwaka 2019/20 matamko yaliyokuwa na dosari yalikuwa asilimia 24. Hata hivyo, kufikia mwaka 2022/23 matamko yenye dosari yalikuwa asilimia 14.
Anaongeza kuwa dosari zilizobainika ni pamoja na: viongozi kutotamka taarifa za fedha katika benki ama kutotamka akaunti namba; na kutotamka kwa ukamilifu taarifa za madeni. Mathalan, kuna baadhi ya viongozi waliotamka kiasi cha fedha wanazodaiwa bila kuonesha ni nani anayemdai. Vilevile, baadhi ya viongozi walipokea zawadi bila kutoa Tamko la Zawadi. Dosari nyingine ni kutotamka taarifa za wenza hasa taarifa za fedha zilizoko benki, kutokujaza baadhi ya vipengele muhimu, kutotamka thamani ya mali, kutokuainisha na kutokutoa ufafanuzi wa vyanzo vya mapato.
KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO YA UKIUKWAJI WA MAADILI
Mkurugenzi huyo anasema kuwa miongoni mwa kazi za msingi za Sekretarieti ni pamoja na kushughulikia malalamiko ya wananchi dhidi ya viongozi wa umma hasa yale yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya mwaka 1995. Katika kipindi cha miaka mitano (5) kumekuwepo na malalamiko dhidi ya viongozi ingawa kasi ama kiwango cha malalamiko kilikuwa kidogo ikilinganishwa na huko nyuma. Uwepo wa malalamiko kwa wingi yanayowasilishwa Sekretarieti unaweza kuwa na tafsiri mbili za usimamizi wa maadili miongoni mwa Viongozi wa Umma.
‘Tafsiri ya kwanza ni wingi wa malalamiko unatokana na Wananchi kuelewa kazi za Sekretarieti na hivyo kuongezeka kwa uwasilishaji wa malalamiko mahali husika. Tafsiri ya pili ni kuwa kupungua kwa malalamiko kuna uhusiano na uelewa kwa wananchi na pia viongozi katika kutekelza majukumu kwa mujibu wa Sheria ya Maadili’ anasema.
Kwa ujumla idadi ya malalamiko yaliyopokelewa na Sekretarieti ya Maadili kutoka Julai, 2019 hadi Aprili, 2024 imepungua kwa kiwango kidogo kutoka malalamiko 234 Juni 2019, hadi malalamiko 226 Juni 2023. Mwenendo huu unaonesha kuimarika kwa ukuzaji maadili na utawala bora nchini.
Pamoja na malalamiko yaliyopokelewa, chunguzi zilizofanywa kwa kipindi cha miaka mitano hasa zile zinazohusu Sheria zimeendelea kuongezeka kwamaana ya kuongezeka kwa rasilimali kwa ajili ya kuchunguza ukiukwaji wa makosa ya kisheria kama inavyoonekana katika mchoro hapo chini.
Anasema kuwa kwa kuzingatia aina ya malalamiko yaliyopokelewa na yale yanayohusu Sheria bado malalamiko kuhusu Matumizi Mabaya ya madaraka, Madai, Matumizi Mabaya ya Rasilimali za Umma yameendelea kuwa changamoto kwa viongozi waliolalamikiwa. Aidha, kwa kada za viongozi zilizolalamikiwa
“Mathalan, katika kipindi cha miaka miwili (2) iliyopita wastani wa uwasilishaji malalamiko kwa mwezi umeongezeka kutoka malalamiko 16 mwaka 2021/22 hadi malalamiko 18 kwa mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 13. Kuongezeka kwa wastani wa malalamiko kunatokana na kuongezeka kwa utoaji wa elimu na hivyo kuongezeka kwa uelewa wa wananchi.
“Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri (Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji) wameendelea kuongoza kwa kulalamikiwa wakifuatiwa na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Meneja. Hata hivyo, kiwango cha ongezeko la kulalamikiwa kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mameneja ni kikubwa zaidi ya asilimia 100. Ongezeko hili kubwa limetokana na ucheleweshaji wa utoaji wa huduma kwa wakati hasa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mchanganuo wa mlinganisho wa malalamiko kwa baadhi ya kada kwa mwaka 2021/22 na 2022/23” anasema.
MABORESHO YA SHERIA YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
Anasema kuwa katika kipindi cha miaka mitano Sekretarieti ya maadili imefanya maboresho makubwa katika kuimarisha utekelezaji wa Sheria ya Maadili. Miongoni mwa maboresho yalifanyika ni pamoja na;Kutungwa kwa Kanuni za Sheria ya Maadili kuhusu Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi (2020/21), Kanuni za Maadili (Mwenendo wa uchunguzi wa malalamiko katika Baraza la Maadili), Kutungwa kwa Kanuni za Sheria ya Maadili kuhusu Ahadi ya Uadilifu (2020/21), Maboresho ya Mengineyo ya Sheria kupitia Gazeti la Serikali Namba 857, na Namba 7 ikijumuisha kuongeza viongozi wanaowajibika na Sheria pamoja na utoaji wa Tamko la Mwisho la Uongozi, kuongeza na kupunguza baadhi ya vipengele ili kuboresha utekelezaji wa Sheria ya maadili.
MATARAJIO YA BAADAYE YA SEKRETARIETI YA MAADILI (THE WAY FORWARD)
Anaongeza kuwa Sekretarieti ya Maadili imejiwekea malengo ya kujenga na kuimarisha maadili ya kitaifa na kuyafanya yawe sehemu ya jamii ili kuzuia mmomonyoko wa maadili katika nchi kwa kujumuisha somo la maadili katika mitaala kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, kufanya marekebisho ya Sheria zinazohusu ukuzaji wa maadili nchini ikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kuboresha Kanuni za Sheria hususan katika eneo la Kudhibiti Mgongano wa Maslahi;
Pia kushirikiana na wadau wengine vikiwemo vyombo vya habari ili kuimarisha maadili kutoka ngazi ya familia hadi ngazi ya taifa, kwani viongozi waadilifu wanatokana na jamii adilifu. Na hapa ndio wanahabari wanahitajika ili kuweza kusaidia kukuza na kusimamia maadili kwa viongozi na wananchi kwa jumla;Kuimarisha mifumo ya kisasa ya Habari na Mawasiliano kati ya Sekretarieti ya Maadili na Wadau. Mfano kuanza matumizi ya online application katika kutoa tamko na kuhakiki mali na madeni ya viongozi;Kupeleka huduma zinazotolewa na Sekretarieti ya Maadili katika ngazi ya Mikoa;Kuboresha Fomu ya Tamko la Rasilimali na Madeni ili ikidhi mahitaji ya sasa; Kusimamia utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma.
Maadili ya uongozi wa umma ni nguzo muhimu ya kuhakikisha viongozi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na uwazi. Wakati wote wa uhai wa Taifa letu, Tanzania imekuwa ikiweka mifumo ya kisheria ya kudhibiti Maadili ya Viongozi. Katika kipindi cha miaka mitano (5), suala la maadili limeendelea kuwekewa mkazo ili kujenga uadilifu, uwajibikaji, uwazi na usikivu miongoni mwa Viongozi na Watumishi wa Umma.
Anasema kuwa lengo la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kuhakikisha kwamba Viongozi wa Umma wanatekeleza majukumu yao kwa namna ambayo inadumisha na kukuza imani na heshima ya wananchi kwa Serikali yao (Ibara ya 8 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977).