Tunakubali rushwa ni adui wa haki? (3)

Katika sehemu ya pili ya makala haya, nilionesha jitihada za Serikali katika kuzuia na kupambana na rushwa nchini, kwa kutunga sheria na kuunda vyombo vya kukabiliana na tatizo hilo.

Tafakari inipa suala zima la rushwa lenye maswali mengi, lakini nimechagua mawili ya awali. Tunakubali rushwa ni adui wa haki? Serikali ina dhamira ya dhati kuondoa rushwa? Hapa naweka msisitizo katika neno dhati ambalo linatawala suala la kutokomeza rushwa.

 

Kamusi ya Kiswahili sanifu toleo la pili inasema “Dhati ni nia thabiti ya kutenda jambo; moyo usiositasita; makini.” Pili inasema “Dhati ni nafsi ya mtu, jambo au mtu.”


Kwa mtazamo wa neno dhati katika maswali hayo kama yatapata majibu chanya, rushwa itatokomezwa. Yakipata majibu hasi rushwa haitaisha.


Yakipata majibu chotara rushwa itaendelea na matokeo ni kuua uchumi wa Taifa letu.

Kuna nukta za kuangalia ndani ya Ripoti ya Tume. Wengi waliotoa maoni na taarifa za rushwa na kutoa ushirikiano mkubwa mbele ya tume, ni wananchi wa kawaida wanaoteseka kiuchumi kutokana na rushwa iliyopo.

 

Wachache waliotoa taarifa za rushwa na ushirikiano dhaifu mbele ya Tume ni viongozi wa kutoa uamuzi wa kitaifa, watendaji wakuu, wanasiasa wakiwamo wabunge. Hawa ni wenye vipato halali, mali na fedha za kutosha.


Leo, viongozi hao hao walioshindwa kutoa ushirikiano kwa Tume, ndiyo wanaosumbua Taifa letu kwenda mrama kiuchumi na wananchi kuishi maisha ya kimaskini na uchoyo.

 

Tume katika ripoti yake imetaja wazi chanzo kikuu cha rushwa nchini kuwa ni uongozi zembe, yaani ukosefu wa miongozo ya wazi juu ya uwajibikaji wa viongozi na mmomonyoko wa maadili ya uongozi.


Aidha, kuibuka kwa mashindano ya matumizi ya kifahari, na mabadiliko katika mazingira ya uchumi huria yametoa hisia, mtu anaweza kufanya lolote na asisailiwe na mtu yeyote.

 

Endapo Serikali kwa maana ya viongozi waandamizi wote, idara na asasi zake kwa pamoja na wananchi wake wangeshirikiana barabara wangeweza kuing’oa mizizi ya rushwa nchini.

Naamini endapo rushwa kabambe itakoma kama si kupungua, basi na rushwa uchwara itakufa kwa sababu inaoteshwa na kuimarishwa na rushwa kabambe.


Nasema hivyo kwa sababu Tume ilipokea maoni na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wa kawaida, jambo ambalo halikupatikana kutoka kwa viongozi, hata hao wachache walijitokeza kwa kusuasua.


Hivi Serikali inapoendelea kutunga sheria, kuweka mipango mkakati na kuunda vyombo vya kupambana na rushwa inatania au inakusudia?

 

Wananchi na vyombo vya habari wanaeleza, wanafichua na kuhadharisha vitendo vya rushwa kwa lengo la kuitaka Serikali ichukue hatua kali kukomesha rushwa, lakini bado rushwa ipo.


Serikali katika baadhi ya maandiko yake inaeleza: “Ni dhahiri pia kuwa ung’oaji kabisa wa rushwa ni lengo la kufikirika tu.” Basi hata kuipunguza kwa asilimia kubwa nalo ni lengo la kufikirika tu?


Nashauri lazima Serikali ‘ijitafune yenyewe’ ndipo tiba ya kweli itakapopatikana.

Adili alijinusuru viboko vya Jalalati Huria kwa kuwachapa viboko nyani (ndugu zake) bila huruma. (Kitabu: Adili na Nduguze – Shaaban Robert). Kwanini Serikali iweke huruma kwa wala rushwa?