Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda amelitaka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha kushirikiana na Mamlaka ya Maji katika kuvitambua, kuviendeleza na kuvitunza visima maalum vya maji vilivyokusudiwa kutumika na jeshi hilo kwenye uzimaji wa majanga ya moto.
Makonda ametoa maagizo hayo leo Mei 20, 2024 kwenye kituo kikuu cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Arusha wakati wa uzinduzi wa magari mawili (2) mapya ya zimamoto na uokoaji yaliyotolewa na serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yakigharimu takribani shilingi bilioni mbili za Kitanzania.
Makonda amesema amebaini kuwa visima vingi vilivyopo mkoani Arusha vimetelekezwa na kutoendelezwa na hivyo amelitaka Jeshi la zimamoto na Uokoaji kuvihuisha na kuhakikisha vinatambulika na vinakuwa tayari muda wote kwa matumizi yaliyokusudiwa na serikali katika kuhudumia wananchi kwenye uokozi.
Halikadhalika Mkuu wa mkoa pia ameitaka Mamlaka ya maji mkoani Arusha kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Jeshi hilo la Zimamoto na uokoaji katika kuongeza visima vya maji kwenye maeneo ya pembezoni mwa mji ambako hakuna visima hivyo vya kutumika kwenye matukio ya uzimaji wa moto.
Mkuu wa mkoa pia ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa mkoa wa Arusha kuzingatia mipango mizuri ya ujenzi wa nyumba pamoja na kuhakikisha kuwa wanatenga maeneo ya barabara za kuingia kwenye maeneo yao pindi ajali mbalimbali zinapotokea.
Mkuu wa mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia magari hayo akisema kuwa hatua hiyo inaendelea kutoa hakikisho la usalama kwa wananchi, wawekezaji na wageni wanaotembelea mkoa wa Arusha.