Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Iringa
Wananchi wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wameishukuru serikali chini ya uongozi wa Rais wa awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa Barabara ya Kidabaga-Bomalang’ombe ambao umeweza kuwaongezea kipato na kuwainua kiuchumi.
Wakiongea kwa wakati tofauti wananchi hao wamesema kwamba baada ya kukamilika kwa Barabara hiyo yenye urefu wa Km. 18.3 wameweza kusafirisha mazao yao hasa mbao, matunda, chai na mbogamboga kwa urahisi.
Bw. Shem Mgunda ambaye ni mkulima wa miti na mkazi wa kata ya Kidabaga ameishukuru Serikali Kwa kuwajengea barabara kwani kipindi cha nyuma wakati wa msimu wa mvua hawakuweza kusafirisha mazao yao kwenda kwenye masoko kwa wakati kutokana na ubovu wa barabara.
Amesema kukamilika kwa Barabara hiyo hivi sasa wanaweza kusafirisha mazao yao na pia barabara hiyo imeweza kuunganisha vijiji vingine na hata magari kwa sasa yanafika hadi sehemu maalumu yakupakia mazao hayo na kusafirishwa.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Kilolo Bw. John Kitweve amesema katika kipindi cha mvua hakukuwa na zao lolote lililokuwa likisafirishwa katika maeneo yao hivyo uchumi wao ulikuwa chini.
Amesema baada ya kutengenezwa kwa barabara hiyo hivi sasa wanafurahia kwani mazao yao mbalimbali yanaweza kusafirishwa kwa wakati na uchumi wa mtu mmoja mmoja umeinuka.
“Mimi kama msimamizi mkuu wa ilani ya CCM nafarijika sana na jitihada za Serikali ya CCM chini ya jemadari Rais Samia Suluhu Hassan. Wilaya yetu ya Kilolo kwa muda mrefu ilikuwa na miundombinu mibovu sana hasa barabara lakini tangu Dkt. Samia aingie madarakani kwa awamu ya sita ya Serikali tumepata maendeleo makubwa sana.” Alifafanua Bw. Kitweve
Aliongeza kusema kwamba miundombinu hiyo imeweza kuwainua wananchi wa wilaya hiyo kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja kwa kiwango kikubwa hata mapato ya halmashauri ya wilaya ukusanyaji wa ushuru unategemea zaidi barabara hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kidabaga Bw. Eusebius Kimata amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwezesha ujenzi wa barabara hiyo na kuongeza kwamba baada ya kujengwa na kukamilika imewasaidia sana kupitisha mazao yao ambapo vijiji vya wilaya hiyo kwa asilimia kubwa wanajishughulisha na zao la mbao.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilolo Mhandisi Mkanda Kidola amesema mradi wa barabara ya Kidabaga-Bomalang’ombe ni wa Km. 18.3 ambapo mradi huo ulitekelezwa katika awamu ya kwanza kwa jumla ya Shilingi bilioni 8.16 na Mkandarasi KIM Builders.
Mhandisi Kidola amesema kwamba kukamilika kwa mradi huo kumeleta faida nyingi kwa wananchi wa wilaya ya Kilolo na pia umekuza uchumi wa eneo hilo pamoja na kuinua maisha ya watu hivyo wanamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapelekea fedha kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara.
Aidha, ameongeza kusema kuwa katika mradi huo pia wamepata muendelezo wa ujenzi wa Barabara ya Km. 1.1 kwa awamu ya pili ambapo ujenzi wake ulianza Mei, 2023 na umefikia asilimia 96 ambapo ujenzi huo unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
“Tunaishukuru serikali kwa Mradi wa Agri- connect kwa awamu zote tatu na tunaona namna wananchi wanavyonufaika na mradi huu hata ukiangalia maisha na uchumi wa watu hao umeongezeka ”.
Ameongeza kusema kukamilika kwa Barabara hiyo imesaidia pia kuongezeka kwa pato kwa serikali na kwa awamu ya tatu mradi huo utaenda kujenga Barabara yenye urefu wa Km. 7.6.” kabla ya ujenzi wa Barabara hii kulikuwa na changamoto kubwa ya usafirishaji wa mazao kwa wakulima kwani mazao yao yalichelewa kufika sokoni”. Aliongeza.
Hata hivyo mhandisi Kidola amesema sasa hivi wananchi wanasafirisha mazao yao kirahisi na kupata faida na kuongeza kwamba kwa Kilolo mjini wametenga fedha za maendeleo kwaajili ya ujenzi Barabara kwa kiwango cha lami kwa Km. 1 ambapo utekelezaji wa ujenzi huo upo katika hatua mbalimbali.
Mradi wa Agri-connect unatekelezwa na TARURA chini ya uratibu wa Wizara ya kilimo kwa ufadhili wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) kwa madhumuni ya kuboresha miundombinu maeneo ya uzalishaji ili kukuza uchumi.