UMOJA wa Mataifa umetahadharisha kuwa zaidi ya watu milioni saba Sudan Kusini watakabiliwa na uhaba wa chakula katika miezi ijayo.
Takwimu hiyo iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ni pamoja na maelfu ya wengine ambao hali yao inatajwa kufikia kiwango cha “janga la njaa.”
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA imesema katika taarifa kuwa, takriban watu milioni 7.1 watakabiliwa na hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa kupata chakula kati ya mwezi Aprili na Julai mwaka huu.
OCHA imeendelea kueleza kuwa jumla ya watu milioni 9 wanahitaji misaada ya kibinadamu Sudan Kusini ambayo katika muda wa mwaka mmoja uliopita, imekuwa chini ya shinikizo kubwa kutokana na vita vinavyoendelea katika nchi jirani ya Sudan.
Tangu vita vilipoanza mnamo mwezi Aprili mwaka jana, takriban watu 670,000 wamekimbilia Sudan Kusini wakitokea upande wa kaskazini.
Kati ya hao, asilimia 80 ni raia wa Sudan Kusini ambao walikuwa wamekwenda kutafuta hifadhi Sudan.
Takriban miaka 13 baada ya uhuru wake mnamo mwaka 2011, Sudan Kusini ambayo ndio nchi changa zaidi duniani, inakabiliwa na misukosuko ya kisiasa, ghasia na ukosefu wa utulivu.