Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar SMZ imesema itaendesha msako na kuzifutia usajili wa wakala wa elimu ya nje ambao wanafanya kazi zao kwa ubabaishaji na kuipongeza Global Education Link GEL kwa mchango mkubwa inaotoa kwenye sekta ya elimu.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein, alipotembelea ofisi za Global Education Link (GEL) zilizoko katika jengo la Thabit Kombo Zanzibar.
Amesema wizara inatambua kazi nzuri zinazofaanywa na baadhi ya wakala kama GEL lakini kuna taaasisi zimeingia kwenye fani hiyo na kufanya kazi kwa ubabaishaji hali ambayo imesababisha malalamiko mengi.
“ Wizara inatambua mchango wa Global Education Link na tunakupongeza tunajua mchango wake kwenye sekta ya elimu mimi najua nilishawahi kuja kwenye moja ya shughuli zako nikajionea ukubwa wa kazi zenu lakini wale ambao hawako makini tutawafutia usajili,” amesema.
Amesema kuna vijana nchini wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekuwa wakirubuniwa na baadhi ya mawakala wa mfukoni wasio waaminifu hali ambayo imesababisha malalamiko mengi.
“Nitatembelea wakala wote na wale ambao hawatambuliki watafunga ofisi lakini GEL tumejiridhisha mnafanyakazi kubwa sana na kwa kweli nimevutiwa na mawazo uliyotushauri kuhusu namna ya kuwasafirisha wanafunzi wengi nje ya nchi kwa kozi ambazo hazipo hapa nchini,” ameaema.
“Mollel tuletee taarifa rasmi kuhusu wazo lako nitaelekeza ofisi yangu iratibu suala hili na kutushauri kwasababu Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ni mwelewa sana anataka mabadiliko ameifanya elimu kuwa kipaumbele kwenye serikali yake siamini kwamba tukimpa wazo hili atalikataa,” amesema.
Amesema Chuo Kikuu Zanzibar SUZA kinachangamoto kubwa ya nafasi kwani uwezo wake ni kuchukua wanafunzi 60 kwenye kozi ya afya wakati wanaooomba kozi hiyo huwa ni zaidi ya 800.
“Tunashindiwa kuwachukua kwasababu hatuna pa kuwaweka na kwa maana hiyo tunakosa wataalamu wengi wa sekta ya afya kwa maana hiyo kuna umuhimu wa kuwapeleka nje ya nchi ili tupate wataalamu wengi wa fani ya afya,” amesema.
Naibu Waziri amesema Rais Hussein Mwinyi anatoa nafasi za vijana kwenda kusoma nje ya nchi kwa hiyo ni wakati mwafaka kwenda kumshauri kuwapeleka nje wale ambao wanakosa nafasi kwenye fani wanazoomba hapa nchini.
“Elimu ambayo nimeipata ndani ya saa moja hapa ni kubwa sana naomba tuendelee kutoa elimu watu wajue wakitaka kwenda kusoma nje ya nchi wafanye nini, serikali tusijifungie tunatakiwa kukutana na wadau wa sekta binafsi kama Global tunapata mawazo mapya,” amesema.
“Wizara tuko tayari kuratibu mikutano ya mara kwa mara baina ya wadau wa serikali na wa sekta binafsi tupeane mawazo mapya, wajumbe wa baraza la wawakilishi nao tuwape elimu wajue mawakala wa elimu ya juu wanafanya nini, Global Education Link anafanya nini, maana wasipoelimishwa wanaweza kudhani ni wale wale wajanja wajanja tu,” amesema.
Amesema hivi karibuni Baraza la Wawakilishi litaanza vikao vyake hivyo atatumia nafasi yake kuitambulisha Global kwa wajumbe wa baraza hilo ili waweze kuwafahamu na wawatumie kwaajili ya kupeleka watoto wao nje.
Alisema ingawa GEL ni ya muda mrefu lakini kuna umuhimu wa kukutana na wadau wengi mara kwa mara na kuwaeleza wanachofanya ili waweze kuwatofautisha na zile taasisi ambazo zimekuwa zikifanya kazi kwa ujanja ujanja.
“Tutakaa na bodi ya mikopo namimi nitaratibu kikao hicho tuone namna yaa kusaidia wanafunzi, tumefungua chuo cha TEHAMA Zanzibar na nia ni kupokea wanafunzi wa kigeni kwa hiyo ni fursa kwenu kuleta wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa GEL, Abdulmalik Mollel, amesema wamezunguma mambo mbalimbali na Naibu Waziri ikiwemo namna ya kuitumia elimu kuakisi uchumi.
Alisema Rais Dk. Hussein Mwinyi amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha uwekezaji kwenye uchumi wa buluu na maono makubwa ya kukuza uchumi wa Zanzibar hivyo kuna umuhimu wa kufanya maandalizi mazuri ya rasilimali watu.