Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha litaendelea kuwashukuru wananchi wanaoendelea kushiriki katika jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira bora na ya kisasa katika vituo vya Polisi mkoani humo huku likibainisha kuwa litaendelea kutoa huduma bora na za kisasa kwa wananchi
Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Peter Lusesa wakati akikabidhiwa ofisi ya Upelelezi Wilaya ya Arushabaada ya kufanyiwa marekebisho na wadau wa masuala ya usalama ili kutoa huduma bora kwa wateja.
ACP Lusesa amesema jeshi hilo kwa sasa nalo limebadilika kiutendaji kutokana na mabadiliko ya kidunia ambapo amewaomba wananchi hao waliojitolea kuboresha ofisi hiyo, watambue kuwa Jeshi hilo litaendelea kutoa huduma bora na za kisasa zinazoendana na mabadiliko ya dunia ya leo.
Sambamba na hilo ACP Lusesa amewataka Maafisa, wakaguzi na askari wanaotoa huduma katika kituo hicho kuhakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wananchi ambao wanalitegemea Jeshi la Polisi huku akiwataka kutambua kuwa Mkoa wa Arusha ndio kioo cha Tanzania katika anga la kimataifa na kitovu cha utali hapa nchini.
Kwa upande wake Nabii Bahati Mwakalinga wa kanisa la Divine Ministry amesema kitu kilicho wasukuma yeye na wenzake ni kutokana na kuona mazingira ambayo sio rafiki kwa wapelelezi katika kufanyakazi yao ambapo waliona ni vyema kukarabati ofisi hizo ili kuwawekea mazingira rafiki kwa askari na wananchi wanaofika kituoni hapo kwa ajili ya huduma.
Nae Mkaguzi Msaidizi wa Polisi A/Insp Anna Mboya ambaye ni Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arusha amebainisha kuwa kwa sasa wanatoa huduma katika mazingira rafiki kitendo kilichosaidia kurahisisha shughuli za upelelezi na kupata ukweli wa Jambo linalopelelezwa.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha Mjini Mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP George Malema amesema kwa sasa kituo hicho kimekuwa ni kituo cha mfano Tanzania ambapo amesema kuwa maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wamekuwa wakifika kituoni hapo kujifunza na kuona maboresho makubwa yaliyofanywa katika kituo hicho.