Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Songea
Huduma za mkoba za madaktari bingwa zinatarajia kuanza kutolewa katika hospitali za Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma kuanzia Mei 6 hadi 10 mwaka huu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk Louis Chomboko amesema timu ya madaktari bingwa 40 ipo mkoani Ruvuma na inatarajia kuripoti kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed Mei 6 mwaka huu kabla ya Kwenda kuanza kazi ya kutoa huduma katika hospitali za Halmashauri.
Dr.Chombo amewataja madaktari Bingwa ambao wapo mkoani Ruvuma kwa ajili ya kuanza kutoa huduma za kibingwa ni Pamoja na madaktari wa magonjwa ya wanawake na uzazi,madaktari bingwa wa Watoto na Watoto wachanga,madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani,madaktari bingwa wa upasuaji na wabobezi wa mfumo wa mkojo na madaktari bingwa wa usingizi na ganzi.
Amezitaja hospitali ambazo madaktari hao watatoa huduma hizo ni Pamoja na hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo,Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga,Hospitali ya Halmashauri ya Madaba na Hospitali ya Halmashauri ya Songea iliyopo Mpitimbi.
Hospitali nyingine amezitaja kuwa ni hospitali ya Wilaya ya Tunduru,hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na kituo cha Afya Mji Mwema kilichopo Manispaa ya Songea.
Natoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza katika hospitali hizo kupata huduma za kibingwa ,serikali imewasogezea madaktari bingwa kwenye maeneo yenu hivyo kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa,mgonjwa anaweza kutumia bima au fedha taslimu’’,alisema Dr.Chomboko.