Na Dotto Kwilasa,
Mkuu wa MKoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, leo Aprili 21, 2024, amefanya mkutano na waandishi wa habari kuutangazia umma juu ya dhamana iliyopewa Mkoa wa Dodoma kuandaa na kufanya maombi na dua ya kuliombea Taifa katika kipindi hiki cha kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania.
Mkutano huo uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma ambao ndipo hafla hiyo itafanyikia mnamo Aprili 22, 2024, Mkuu wa MKoa ametoa hamasa kwa waumini wa Madhehebu ya dini zote na wananchi wote wa Dodoma kufika kwenye uwanja huo kuungana na viongozi wa dini mbalimbali watakaoshiriki maombi hayo.
“Heshima tuliyopewa ni kubwa na inapaswa kuthaminiwa na wanadodoma na tunatakiwa kuonesha thamani hii kwa kujitokeza kwa wingi, tujae uwanjani hapa ili kufanya maombi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Muungano kuendelea kuimarika lakini pia kuuombea Muungano wetu uendelee kuwa wa mfano.
Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa maombi haya ni kwa ajili ya kuombea tudumu katika umoja, amani na utulivu kama ilivyo historia yetu kutoka kwa waasisi wa Muungano huo. Aidha, wanadodoma wanaotarajiwa kushiriki maombi hayo wanafikia 30,000 hivyo, shime imetolewa kwa wananchi wote kufika na kushiriki pamoja.
“Tuhamasishane sote kufika hapa kwani maombi huleta Baraka. Tujitokeze kwa wingi ili tuendelee kuifaharisha Dodoma kwa matendo haya makubwa. Karibuni pia mikoa ya jirani tufanye maombi kwa ajili ya Taifa letu” Amesisitiza Mhe. Senyamule.
Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango. Tukio hilo litaanza saa 1:00 asubuhi kwa wananchi kuanza kuingia viwanjani hapo.