Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeunga mkono jitihada za Serikali katika kuchangia matibabu ya wagonjwa wa saratani katika Taasisi ya Saratani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana.
Akizungumza wakati wakukabidhi misaada mbalimbali kwa Taasisi hizo, Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema kuwa Mamlaka imeona vyema kutoa msaada huu kwa wagonjwa wa saratani kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa wa saratani kuweza kukidhi matibabu yao.
Amesema kuwa mamlaka imeona uhitaji mkubwa wa matibabu ya wagonjwa hawa wa saratani kwa kuwa wengi wao hawajawa na uwezo wa kukidhi gharama kubwa za matibabu yao.
“Tumeona namna ambavyo wagonjwa wengi wameshindwa kugharamia matibabu yao kutokana na gharama kuwa kubwa, hivyo tumeona tuwawezeshe kwa kugharamia matibabu yao,” ameeleza Mhandisi Mtindasi.
Sambamba na kuwezesha gharama za matibabu, mamlaka pia imekabidhi misaada ya kibinadamu kwa wagonjwa wa Amana na Taasisi ya Saratani ili kusaidia wagonjwa kuweza kukidhi mahitaji yao binfasi.
Akipokea msaada huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana Dkt. Bryceson Kiwely ameishukuru Mamlaka kwa jitihada zao za kuwasaidia wagonjwa kukidhi mahitaji yao na kuwagharamikia matibabu yao kwa kuwa wengi wameshindwa na kusababisha kushindwa kupona.
“Msaada huu uwe chachu kwa watu wengine, Taasisi, vikundi mbalimbali na wadau wengine kuona haja ya kuwasaidia watanzania wenzetu ili waweze kupata unafuu wa gharama za matibabu yao,” ameeleza Dkt. Kiwely.
Nae Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Bi Kway ametoa pongezi zake za dhati za uongozi mzima wa Mamlaka kwa kuguswa na jambo hili na kuona huruma ya kuwasaidia wagonjwa wa saratani katika kukidhi mahitaji yao.
“Hili ni jambo la baraka hasa kwa kuwa tunaokoa maisha ya mtanzania mwenzetu ambae ameshindwa kumudu gharama za matibabu, kwa kufanya hivi inasaidia pia kuunga mkono jitihada za Serikali za kuokoa uhai wa Watanzania walio wengi,” ameeleza Bi Irene.