Ujasiriamali unahitaji ‘roho ya paka’

Ninafahamu linapokuja suala la matumizi ya Kiswahili katika mambo ya biashara na ujasiriamali, akili zetu zinapwaya. Sio kwa sababu Kiswahili hakina maneno yote ya kibiashara, la hasha! Ni kwa sababu hatujazoea biashara, misamiati haijatukaa sana kama ilivyotukaa ya kisiasa. Moja ya neno nililokopa kama lilivyo ni ‘Risks’; na ndio dhana nitakayoijadili leo.

Ujasiriamali unahitaji mtu awe na roho ya paka (roho ngumu na ya uvumilivu mkubwa). Leo kupata faida na kesho hasara, ama kufilisika kabisa, ni mambo ya kawaida. Wajasiriamali wengi tuna tatizo katika utunzaji na ukuzaji mitaji.


Yaani, mitaji inapanda na kushuka. Mtu unaweza kufanya biashara akafikisha labda mtaji wa Sh milioni 20 lakini baada ya muda fulani unashangaa mtaji unabaki Sh milioni 10. Inakuwa kama mchezo wa kubahatisha (kupata ama kukosa). Wakati mwingine wajasiriamali tunaishi kwa misongo mikubwa kimawazo kutokana na mambo kwenda ndivyo sivyo. Unaweza kuchukua mkopo benki halafu biashara ulizotegemea zikakataa.


Ikiwa uliweka dhamana ya nyumba, ama rasilimali nyingine, lazima jasho lianze kukutoka. Wakati mwingine unaweza kufanikisha kulipa mkopo lakini ukajikuta mtaji haujaongezeka, na pengine umeshuka; inakuwa kama ulikuwa unaizalishia benki!


Uzoefu unaonesha kuwa usipokuwa makini katika ujasiriamali, unaweza kushindwa hata kumudu ndoa yako. Kufanikiwa kibiashara inatakiwa kuendane na furaha katika familia na ustawi wa afya ya mwili wako. Unatakiwa kuwa na fedha ya kutosha na muda wa kutosha kupumzika, ama kukaa na familia yako.


Kinachosikitisha ni kuwa wajasiriamali wengi wanakuwa na fedha, lakini hawana muda wa kufurahi na familia wala ndoa zao. Hata wanapokuwa katika nyumba zao akili zao haziwi kwa wake na watoto wao, zipo kwenye ujasiriamali, ama zinawaza marejesho ya mikopo! Wajasiriamali wengi hawajui ni lini hasa watakuwa na furaha za kudumu. Kuwa na furaha katika maisha yao ni kama bahati nasibu!


Kupanda na kushuka kimafanikio, kuishi na vidonda vya tumbo, ama presha kunakotokana na mawazo; pamoja na migogoro ya kifamilia sio stahili ya mjasiriamali na haifai kuwa hivyo. Pamoja na hayo, mazingira ya ujasiriamali tuliouzoea Tanzania yanatusababisha kuwa katika hali hizi, Je, tunajikwamuaje hapa?


Ili kuepuakana na hali za ujasiriamali kuwa kama mchezo wa kubahatisha kuna mtindo wa kufanya biashara ambao wajasiriamali tunatakiwa kuuzoea. Ni kuwekeza katika aina tofauti za biashara kwa wakati mmoja.


Kwa kitaalamu mtindo huu tunauita ‘diversification’ ambapo biashara mbalimbali unakowekeza zinaitwa ‘portofolio’. Kufanya ‘diversification’ kunaondoa kubahatisha katika kupata faida, kunapunguza msongo wa mawazo na kunakupa furaha ya  ujasiriamali muda wote.


Kwa mfano, badala ya kuhangaika na biashara ya mbao pekee, ambayo ina mtindo wa kupanda na kushuka (kutegemea na msimu), ni vema mjasiriamali ukawekeza katika biashara nyingine kama vile majengo, usafirishaji na nyinginezo. Kanuni  itakayokusaidia katika ‘diversification’ ni kuhakikisha biashara unazowekeza zisifanane, ama kutegemeana.


Ukiwa mfanyabiashara wa mazao, ‘diversification’ haitakuwa na tija kubwa kama utawekeza katika usafirishaji kwa kununua lori. Shida itakuwa ni moja, biashara zako zote mbili zitakuwa ni za msimu; msimu wa mazao ukiisha na biashara ya usafirishaji itasimama (ikiwa lori hukodishwa kusafirisha mazao).


Ndio maana ninasema katika kufanya ‘diversification’ mjasiriamali unatakiwa kutafuta biashara ambazo angalau moja inapoenda vibaya basi nyingine iwe inazalisha faida. Ukianza na kujizoesha kufanya ‘diversification’ haimaanishi hautapita katika changamoto za kuyumba, lakini nakuthibitishia kuwa hautakuwa mtu wa kuyumba kiasi cha kufika sifuri.


Najua kuna watu watawaza mioyoni mwao mambo mengi kuhusu hii ‘diversification’. Unaweza kuniuliza, “Nitafanyaje biashara zaidi ya moja na mtaji unanikaba?” Ama unaweza kujisemea, “Biashara zaidi ya moja nitasimamiaje?” Kuhusu la usimamizi nitalieleza katika makala zijazo, lakini hili la mtaji ni rahisi.


Usisubiri kuwa na mtaji mkubwa ili ufanye ‘diversification’. Pale ulipo angalia ni biashara aina gani tofauti unaweza kuzifanya kwa wakati mmoja? Kwa mfano, unaweza kuwa na mgahawa wenye mtaji wa laki tatu halafu ukawa na ‘salon’ yenye mtaji wa laki tano, tayari hii ni ‘diversification’.


Hata katika mikopo, huwa rahisi kwa mjasiriamali kurejesha mkopo kwa wakati ikiwa una biashara zaidi ya moja. Kuna wakati itatokea, biashara uliyochukulia mkopo ikagoma, lakini ukaweza kurejesha mkopo kupitia biashara nyingine. Lakini ukiacha hilo, mjasiriamali unakuwa na maisha yasiyo na mawazo ya kuumiza, unakuwa na uhakika kwa unayoyafanya.


Tatizo la wajasiriamali wengi ni ubishi wa kung’ang’ania biashara moja miaka nenda rudi, na kuigana. Biashara iliyokufaidisha jana sio lazima ikupe faida leo. Biashara inayompa faida mwenzio haimaanishi ukianzisha na wewe utapata faida.


Mazingira yanabadilika, ushindani unaongezeka, hivyo ni lazima kukabili changamoto mpya na kuwa tayari kujaribu biashara mpya. Hili litasaidia mjasiriamali kuwa na uhakika kwa biashara zako na kuepuka maisha ya kubahatisha kiujasiriamali! Tuonane wakati ujao.