Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi kuhakikisha zinazingatia matakwa ya sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.
Rais Samia amesema hayo leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa binafsi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere.
Aidha, Rais Samia amesema Tume hiyo imeundwa kwa mujibu wa Katiba ili iweze kulinda haki na maslahi ya raia nchini na kukamilisha wajibu wa nchi kikanda na kimataifa.
Rais Samia pia amesema maendeleo makubwa ya kiteknolojia yanaweza kusababisha kukusanywa kwa taarifa binafsi za watu, kuchakatwa na kutumika bila wahusika kufahamu.
Vile vile, Rais Samia amesema licha ya uwezekano wa taarifa binafsi kutumika kwa hujuma lakini pia taarifa binafsi ni biashara kubwa kwa makampuni mbalimbali ya kimtandao.
Kwa upande mwingine, Rais Samia ameitaka ofisi ya Waziri Mkuu kushirikiana na Wizara husika kusimamia na kuhakikisha mifumo ya TEHAMA yote nchini inasomana ili ifikapo tarehe 31 Desemba, 2024 itumike namba moja kwa masuala ya utambulisho.
Umoja wa Afrika kupitia Mkataba wa Malabo wa mwaka 2014 unasisitiza ulinzi wa faragha huku Jumuiya za Kikanda zikizitaka nchi wanachama kulinda uhuru huo kwa kutunga Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya Miamala ya Fedha ya Kielektroniki na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.