Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia. Pwani
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ambae pia ni Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini ,Dkt.Tulia Ackson ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete kuwapa pole mashabiki wa Simba waliopata ajali Machi 29 ,Vigwaza Mizani, Chalinze mkoani Pwani.
Katika ajali hiyo watu wawili walifariki dunia na wengine 25 kujeruhiwa kati ya waliojeruhiwa wanaume 18 na wanawake saba ambapo wamepatiwa matibabu katika hospital ya wilaya Chalinze huku wanne kati yao wamefikishwa hospital ya Muhimbili MOI kwa matibabu zaidi.
Tulia Ackson ametoa rambirambi yake ya sh milioni 2 na majeneza mawili kwa ajili ya kuhifadhia miili ya marehemu.
Aidha mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete,amechangia milioni 3.5 kwa ajili ya kulipia matibabu kwa majeruhi wote waliotibiwa hospitali ya Msoga.
Vilevile Waziri Mkuu,Majaliwa Kassim Majaliwa amechangia milioni moja huku klabu ya Simba ikichangia matibabu ya majeruhi waliopo Muhimbili na kusimamia taratibu za kusafirisha miili na wagonjwa walioruhusiwa.
“Alipangalo mungu halina makosa tumewapoteza wenzetu wawili,na majeruhi wakiendelea na matibabu kikubwa marehemu tukawapumzishe katika Nyumba Yao ya milele salama na tuendelee kuwachangia wenzetu ambao wanaugua kwa majeraha warejee katika hali zao za kawaida”alifafanua Ackson.
Mbunge Ridhiwani Kikwete aliwapa pole majeruhi na kueleza,madeni yote yanayohitajika kulipiwa hospital ya Msoga analipia yote .
Msemaji wa Simba sports Club ,Ahmed Ally alieleza ilikuwa ni safari ya kwenda kuipigania Simba ,hivyo ni lazima kushirikiana na ndugu na Jamaa wa marehemu na majeruhi bega kwa bega.
“Umoja wetu ni nguvu,walionyesha nguvu yao,wamepata Janga wakiwa wanaitetea Simba ,hatuna budi kushirikiana,ni hii ndio nguzo ya Simba Umoja wetu kwanza ,na ajali hii isisababishe uoga kwa mashabiki kushindwa kusafiri kwenda kushabikia timu yao kwa kuogopa ajali ,kwani ajali hupangwa na mungu na inakufika popote muda wako ukifika “alisisitiza Ahmed.
Waliofariki katika ajali hiyo ni Oleison Mwakasila, anaekadiriwa kuwa na miaka 42-45, mkazi wa Kiwila mkoani Mbeya na Dereva wa gari hilo dogo aina ya kosta aitwaye Moses Mwaisela, mwenye umri kati ya miaka40-43, mkazi wa Uyole.