Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema kuwa katika kipindi cha katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utatuzi wa hoja za Muungano umeendelea kuimarika.
Amesema Serikali zote mbili zimeweka Mwongozo rasmi wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya Kushughulikia Masuala ya Muungano ambavyo hushirikisha wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano ambavyo hufanyika katika ngazi za Makatibu Wakuu, Mawaziri na kikao cha Kamati ya Pamoja ambacho Mwenyekiti wake ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, jijini Dodoma leo Machi 26, 2024, Dodoma, Dkt. Jafo amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya pamoja mwaka 2006, hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 25 zilizoibuliwa.
Amesema hoja nyingi ambazo zilikuwa hazijapatiwa ufumbuzi zimejadiliwa na pande zote mbili za Muungano na kupatiwa ufumbuzi ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 pekee hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo kwa kipindi hicho. Hoja zilizobakia zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.
Waziri Jafo amesisitiza katika kuhakikisha usawa wa utoaji wa huduma kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano, Taasisi za Muungano zilizopo Tanzania Bara zimefungua Ofisi Zanzibar ambapo hadi sasa Taasisi 33 zimefungua Ofisi Zanzibar kati ya Taasisi 37 za Muungano.
Kwa upande wa Mazingira amesema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 na baadaye Sera ya Mazingira ya mwaka 2021 ambapo mafanikio makubwa yamepatikana katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuratibu utekelezaji wa Kampeni ya Upandaji Miti nchini ambapo kila Halmashauri ya Wilaya imeelekezwa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.
Kuhusu huduma mbalimbali za kijamii, Waziri Dkt. Jafo amesema kabla Muungano shule za msingi zimeongezeka kutoka 3,270 hadi 20,562 mwaka 2024 ambapo kati ya hizo za Serikali ni 18,012 na za binafsi ni 2,550.
Vilevile amesema shule za sekondari zimeongezeka kutoka 41 mwaka 1961 hadi 6,511 mwaka 2024 ambapo kati ya hizo, shule 4,892 ni za Serikali na 1,619 ni za binafsi.
Kwa upande wa huduma za afya amesema vituo vya kutolea huduma za afya ngazi zote vimeongezeka kutoka 1,343 mwaka 1960 hadi vituo 9,662 mwaka 2024 na kati ya hivyo ni zahanati 8,043, vituo vya afya 1,176, hospitali za halmashauri 171, hospitali zenye hadhi ya wilaya 182 na hospitali za rufaa za mikoa 28.
Ameongeza hospitali zenye hadhi ya Mkoa 34; Hospitali za Rufaa za Kanda 5; Hospitali zenye hadhi ya Kanda 11; Hospitali maalumu 6; Hospitali ya Taifa 1; na Hospitali Maalumu za Taifa 6.
Aidha, Dkt. Jafo ametaja mafanikio mengine ni kuimarika kwa upatikana wa huduma za maji, umeme na mtandao wa barabara, upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 32 mwaka 2000 hadi asilimia 77 mwaka 2022.
Aidha, upatikanaji wa umeme umeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2000 hadi 78 mwaka 2022. Vile vile, mtandao wa barabara za lami na zege mijini na vijijini umeongezeka kutoka KM 1,360 mwaka 1961 hadi KM 11,966 mwaka 2022.
Hivyo, amesisitiza tangu kuasisiwa kwa Muungano wetu miaka 60 iliyopita, kumekuwa na faida nyingi zinazoufanya Muungano uendelee kuimarika na kushamiri na msukumo na kipaumbele cha uhifadhi na usimamizi wa Mazingira ukiendelea kutolewa na Viongozi Wakuu wa Serikali.