Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo anatarajiwa kuongoza mapokezi ya ndege mpya ya abiria aina ya Boeing 737-Max9 yenye uwezo wa kubeba abiria 181.
Ndege hiyo itapokewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam ikitoka nchini Marekani ilikokuwa inatengenezwa.
“Ndani ya miaka mitatu, serikali imenunua ndege tano mpya zikiwemo tatu za masafa ya kati aina ya Airbus A220 mbili na Boeing 737-Max9,” ameeleza Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali mwishoni mwa Juma katika mkutano wake na vyombo vya habari.
Matinyi amesema nyingine ni Boeing 767-300F ya mizigo na Dash 8Q-400 na zinaendelea kutoa huduma.
Amesema Boeing 737-Max 9 iko kwenye hatua ya makabidhiano na nyingine ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8 iko katika hatua ya
uundwaji.
“Sasa ATCL ina jumla ya ndege za abiria 12 na moja ya mizigo zinazohudumia vituo 24 vya sasa kutoka vituo 19 mwaka 2021 na inatara-jiwa vitaongezeka,” amesema.
Matinyi ameeleza kuwa kwa ujumla, ATCL imeongeza idadi ya abiria kutoka 537,155 mwaka 2021 hadi 1,070,734 kwa sasa na kwa upande wa mizigo mwaka 2021 ilibeba tani 1,290 sasa zimefika tani 3,561.