Na Suzy Butondo,JamhuriMedia, Shinyanga
Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu waliokuwa wakiendesha shughuli zao za uchimbaji kwenye mgodi uliopo kijiji cha Imalamate Wilaya ya Busega mkoani Simiyu wameamua kumfungulia mashitaka rais wa Chama cha Wachimbaji wa madini Tanzania (FEMATA), John Bina kwa kushindwa kuwalipa fidia ya maduara yao baada ya kufukiwa kwenye mgodi anaoumiliki.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana mjini Shinyanga muda mfupi baada ya kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga wachimbaji hao wamesema uamuzi wao huo unatokana na rais huyo kushindwa kuwalipa fidia baada ya maduara yao kufukiwa kwenye mgodi huo.
Wachimbaji hao wamesema pamoja na kwamba wao ndiyo waliogundua uwepo wa dhahabu katika kijiji hicho cha Imalamate, lakini katika njia ambazo hawakufahamu walipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwamba eneo hilo lina leseni ya John Bina.
Wamesema kwa vile wao ni wachimbaji wadogo na hawakuwa na uwezo wa kukata leseni walikubali kukaa pamoja na rais huyo na wakawekeana taratibu za kuendelea kuchimba madini ya dhahabu kwa kutumia leseni yake, ambapo katika mapato waliyoyapata asilimia 30 walimlipa John Bina.
Wachimbaji hao wamedai kuwa wakati wakiendelea na uchimbaji kuna wakati baadhi ya maduara yaliporomoka na kusababisha vifo vya baadhi ya wachimbaji, ambapo Serikali kupitia Tume ya Madini ilitoa maelekezo ya kuimarisha eneo lote la machimbo ili kuepuka maafa kutokea tena barua ya maelekezo hayo alikibadhiwa mmiliki wa mgodi ambaye pia ni Rais wa FEMATA.
Mwenyekiti wa wachimbaji ambao maduara yao yalifukiwa, Jumanne Guguyu amesema jambo la kushangaza mnamo Aprili 28, 2022 waliona timu ya Jeshi la Polisi wakiwa na magreda makubwa yalifika kwenye mgodi wao na kuanza kufukia maduara yote yaliyokuwa kwenye eneo hilo bila ya wao kupewa taarifa yoyote.
“Hivyo amesema tumeamua kumfungulia mashitaka mahakamani Rais wa FEMATA, John Bina baada ya maduara yetu yaliyokuwa kwenye mgodi wake kule Wilaya ya Busega, mgodi Dutwa namba mbili kijiji cha Imalamate, tumechukua uamuzi huu baada ya kupitia kila sehemu kufikisha malalamiko yetu kuanzia Serikali ya kijiji hadi kwa mkuu wa mkoa.” amesema.
“Huko kote huko hatukupata msaada wowote, hivyo tulikwenda Tume ya Madini Dodoma, ambao walitoa maelekezo kwa John Bina, miongoni mwa maelekezo hayo ni kututafutia eneo mbadala jirani na mgodi wake ili tuendelee kuchimba madini, lakini hakutekeleza maelekeza hayo,” alieleza Guguyu.
Guguyu aliendelea kueleza kuwa kwa sasa wao wanachokidai ni kulipwa fidia ya maduara yao yaliyofukiwa ambapo katika ufukiaji huo walipoteza mali zao zote na wakapata hasara zaidi ya shilingi bilioni 3. na hivi sasa wengi wao hawana pa kushika huku wengine wakidaiwa mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha.
Modesta Robinson, Happiness Balile na Sospeter Maduhu pia ni miongoni mwa wachimbaji wadogo ambao mashimo yao yalifukiwa mbali ya kwenda mahakamani wamemuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa madini Anthony Mavunde wawasaidie ili kuona haki yao inapatikana.
“Katika mgodi ule tulikuwa tumewekeza mali nyingi, ilikuwa ni busara kabla ya uamuzi wa kufukia maduara yetu tungeshirikishwa kwanza, maana awali tuliwahi kusikia, Bwana Bina anataka kuwauzia wawekezaji wa Kichina, tulipomuuliza alikana na kudai siyo kweli, na amesema tuendelee na shughuli,”
“Sasa tulishangaa kuona tunafukuzwa na siku maduara yetu yanafukiwa hatukuruhusiwa hata kusogea karibu kwa vile shughuli ilisimamiwa na askari Polisi waliokuwa na silaha nzito, kwa kweli tulilia sana, tunamuomba Rais pia awatupie macho viongozi wetu hawa, huyu alikuwa mwakilishi wetu, lakini alitusaliti,” ameeleza Maduhu.
Wachimbaji hao walisema wanashangazwa kuelezwa kuwa mgodi ulifungwa kwa sababu za kiusalama wakati tayari yupo mwekezaji wa kichina anayedaiwa ndiye aliyeuziwa mgodi huo na Rais wa FEMATA akiendelea na shughuli za uchimbaji bila matatizo.
Kwa upande wake Rais wa wachimbaji John Bina akizungumza kupitia simu yake ya kiganjani, alikanusha kufukia maduara ya wachimbaji hao na kufafanua kuwa ufukiaji huo ulifanywa na uongozi wa Serikali chini ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa baada ya kutokea maafa ya mara kwa mara na hivyo kuagizwa mgodi ufungwe.
“Kwanza suala la watu kwenda Mahakamani ndiyo sehemu pekee ya kutafsiri haki, na mimi Bina kama Bina siko juu ya sheria, lakini nataka nikuhakikishie kwamba eneo lile hakufukia Bina, wao watakuwa wamewadanganya tu, maagizo yale yalitolewa na Tume ya Madini baada ya kuongezeka kwa matukio ya maafa kwenye mgodi ule,”
“Tume ya madini kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, TAKUKURU na usalama wa Taifa ndiyo waliosimamia zoezi la ufukiaji, kwa hiyo nikaathirika mimi mwenye mgodi pamoja na wachimbaji wengine zaidi ya elfu moja waliokuwepo pale pia waliathirika, suala la kwenda mahakamani ni utashi wao,” alieleza Bina.
Amesema awali kesi hiyo ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, ambako hata hivyo Mahakama hiyo ilitupilia mbali madai yao baada ya kuona hayakuwa na msingi na kwamba kama wameamua kufungua tena basi wakati utaongea huku akikiri yeye ndiye aliyekuwa mmiliki wa leseni kwenye mgodi huo.