Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeanza kutoa mafunzo ya siku tatu kwa wawakilishi kutoka nchi za Burundi na Sudan Kusini juu ya utoaji wa huduma za urasimishaji wa biashara kwa njia ya mtandao katika Ofisi za taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho Manongi, akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwafundisha wawakilishi hao namna ya kutumia mifumo ya Usajili ili wakatumie ujuzi huo katika kuanzisha na kuendeleza mifumo kwenye nchi zao.
“Katika moja ya mambo makubwa ambayo Serikali imefanya ni kuunganisha mfumo mmoja wa kuwezesha kusajili biashara na kupata Leseni, uliowezesha kufanya vizuri zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kupelekea nchi ya Sudan Kusini na Burundi kuja kujifunza” amesema Bw. Manongi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amefurahishwa na ujio wa ugeni huo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kwa kuiona Tanzania kupitia taasisi ya BRELA kuwa imepiga hatua upande matumizi ya mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao hii inaonesha wazi kuwa kazi kubwa inafanyika katika uwezeshaji na urasimishaji wa biashara nchini.
“Sisi tutawapitisha na kuwaonesha mifumo yetu hatua kwa hatua namna mfanyabiashara anavyosajili hadi afisa anavyochakata maombi mbali na hayo tunatarajia kutengeneza mashirikiano ya kufanya kazi ili sisi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki tuweze kuongea lugha moja” amesema Bw.Nyaisa.
Naye Mwakilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Uwekezaji Bw. Charles Omusama amesema nchi hizi mbili zipo kwenye machakato wa kuanza kutoa huduma za usajili kwa njia ya mtandao hivyo Tanzania imeonekana ni nchi iliyopia hatua katika utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo.
Aidha, Kaimu Msajili Mkuu wa Kampuni za Biashara kutoka Wizara ya Sheria Sudan Kusini Bw.Madol Anyuat amesema kuwa wapo Tanzania kwa ajili ya ziara ya mafunzo kwa vitendo ili waweze kuona namna mifumo ya sajili inavyofanya kazi ili watakaporudi watachukua hatua ya kuanzisha mifumo ya kusaidia ukuaji wa sekta ya biashara.
Naye Bi.Alida Mugisha, ameeleza kuwa nchi ya Burundi imeanza kutumia mifumo ya usajili mwaka 2022 ila bado wanakumbana na changamoto mbalimbali, kwa kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa hivyo ziara hii itawajengea uwezo ili waboreshe katika nchi yao.
Mafunzo haya yaliyoanza leo yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku tatu yatakwenda sambamba na mafunzo kwa njia ya vitendo pamoja na kutembelea wadau wakubwa wanaotumia huduma za BRELA.