Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali imesema kuwa itaendelea kujenga mahusiano mazuri na waendesha bajaji na pikipiki maarufu kama bodaboda pamoja na kushiriana nao kwani kazi hiyo ni kama kazi zingine.
Hayo yameelezwa leo Machi 25, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo wakati akifungua semina ya Elimu kwa Mlipakodi ilioandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa viongozi wa mashirikisho ya waendesha vyombo vya moto kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
“Niwapongeze TRA kwa kuandaa mkutano na watu hawa kwani ni imani yangu baada ya kuwapatia elimu hii kwa mlipakodi tutaendelea kujenga ushirikiano mzuri.
“Serikali inatambua kazi ya bodaboda na bajaji ni kama kazi zingine hivyo sisi kama serikali tutaendelea kuwatambua na kuwajali. Niwaombe ninyi viongozi mliofika hapa leo kupokea mafunzo haya kutoka kwa TRA mkawe mabalozi kwa wenzenu,” amesema Mpogolo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano TRA, Hadson Kamoga amesema mafunzo hayo yamehusisha viongozi wa waendesha bodaboda na bajaji ambao ni watu muhimu na wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kuendesha uchumi wa miji mikubwa.
“Kwenye suala la kodi yapo mambo mbalimbali ambayo wataelimishwa mojawapo ni umiliki wa kile chombo wanachokitumia hususani kwa wale wanaopewa vyombo vya mikataba.
Tumegundua kuna changamoto ya kutumia chombo ambacho hakina umiliki wake yeye, chombo ni cha kwake lakini tangu alipokabidhiwa baada ya mkataba hajafanya uhamishaji wa umiliki ambapo kadi inasoma jina lingine lakini chombo ana miliki yeye.
“Kwahiyo inapotokea changamoto anashindwa kupata haki yake, lakini pia suala la leseni utakuta kuna changamoto waendesha bodaboda na bajaji hawaoni umuhimu wa kuwa na leseni. Na pia wanatakiwa kutambua kuwa kodi zipo kisheria na ni sehemu ya maendeleo, ingawa tumegundua sio kwamba hawataki kulipa kodi, ni kutokana na kutokuwa na elimu,” amesema Kamoga.
Mwenyekiti wa bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Said Kagomba amesema: “Tunaishukuru TRA kwa elimu hii ya mlipakodi, pamoja na matumizi ya vyombo vya mkataba. Tunawaomba isiwe ndo mwisho, elimu hii inatakiwa ienee kila mahali, hii itaondoa manung’uniko ili nchi yetu iweze kusonga mbele,” amesema.