Na Lilian Lundo – Maelezo
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato tangu imeingia madarakani.
Bw. Matinyi amesema hayo leo Machi 24, 2024, jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari, kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kufanya vizuri katika kipindi cha miaka mitatu hii kwa kufuata mwongozo wa Rais wa kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara na kujali changamoto wakati wa kukusanya kodi. Hivyo basi, makusanyo yamefikia shilingi trilioni 24.14 kwa mwaka 2022/23 kutoka shilingi trilioni 18.15 mwaka 2020/21. Hili ni ongezeko la shilingi trilioni 5.99,” amesema Bw. Matinyi.
Ameendelea kusema kuwa, kwa mwezi Desemba 2023, TRA ilivunja rekodi ya ukusanyaji ya kila mwezi baada ya kufanikiwa kukusanya shilingi trilioni 3.05 licha ya kuwa wastani kwa mwaka huu hadi sasa ni shilingi trilioni 2.13. “Ni vema kufahamu kwamba hadi kufikia tarehe 20 Machi, 2024, TRA ilikuwa imeshakusanya kiasi cha shilingi trilioni 19.21, ikiwa ni dalili mkwamba itavuka kiasi cha mwaka uliopita,” amefafanua Bw. Matinyi.
Amesema, kwa upande wa uwekezaji katika kipindi cha Machi 2021 hadi Machi 2024 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimefanikiwa kusajili jumla ya miradi 1,188 ambayo ilikadiriwa kuwekeza kiasi cha mtaji wa dola za Marekani milioni 15,041 na kutoa jumla ya ajira 345,464. Kati ya miradi hiyo asilimia 35 inamilikiwa na watanzania, asilimia 41 ni ya wageni na asilimia 24 ni ya ubia kati ya watanzania na wageni.
Vilevile, thamani ya uwekezaji katika taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina imeongezeka kutoka shilingi trilioni 70 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 76 mwaka 2023, sawa na ongezeko la 8.6%.
Sababu ya ongezeko hilo ni Serikali ya Awamu ya Sita kuongeza mitaji kwa kiasi cha shilingi trilioni 5.5 katika mashirika ya kimkakati kwa maslahi ya taifa.
Aidha, ofisi hiyo pia imeongeza makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kutoka shilingi bilioni 637.66 hadi trilioni 1.008 kwa mwaka 2023, sawa na ongezeko la 58%. Serikali pia imeongeza umiliki wa hisa katika kampuni ya almasi ya Williamson Diamonds kutoka asilimia 25 hadi 37 huku ikisaini mikataba ya ubia wa asilimia 16 zisizohamishika katika kampuni za madini.