Waongoza utalii Mkoa wa Arusha,wametoa siku saba kwa rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili ili kufikia malengo ya Serikali iliyojiwekea katika sekta ya utalii.
Akiongea kwenye mkutano wa pamoja uliokutanisha vyama mbalimbali vya waongoza utalii nchini,Mwenyekiti wa mkutano huo, Abdallah Noar, amesema moja ya changamoto hizo ni pamoja na kutakiwa kulipa leseni na viingilio pindi wanapoingia kwenye hifadhi .
Amesema wao ni sehemu ya watumishi katika sekta ya utalii hivyo hawapaswi kulipia viingilio wanapoingia kwenye ofisi zao ambazo ni hifadhi za Taifa.
Noar amesema Machi 7, mwaka huu , walipokea barua kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ,inayowataka waongoza utalii kote nchini ifikapo Mei 1,mwaka huu mfumo wa kudhibiti waongoza utalii wasio na leseni kuingia hifadhini, utaanza kutumika rasmi.
Amesema barua hiyo inalenga kutekeleza mfumo wa kuthibiti waongoza watalii wasiokuwa na leseni ya biashara (TTBL) .
Sehemu ya barua hiyo inasema kuwa sheria ya Utalii Na.29 ya mwaka 2008 kifungu cha 42(1)kinaelekeza kuwa kila mwongoza utalii anapaswa kusajiliwa kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa katika kifungu cha 42(2).
Mwenyekiti huyo ambaye amemtaja Rais Samia kama mwongoza utalii namba moja nchini, wamemwomba kuwasaidia kuondoa changamoto hiyo ambayo wanadai inawaumiza katika shughuli zao.
Wadau hao wa utalii kwa pamoja wametoa wiki mbili kwa rais Samia kutatua kero hiyo na baada ya muda huo kwisha bila majibu sahihi wataitana tena ili kupata kauli nyingine ya pamoja watakayokubaliana.
Amesema kuwa sheria hiyo ilipitishwa na Bunge mwaka 2008 lakini ilikuwa haifanyi kazi hadi juzi walipoiibua upya, hata hivyo alisisitiza kuwa sheria hiyo haikuwa shirikishi na inamapungufu mengi ukizingatia kuna watu wengi wanafanyakazi kwenye hifadhi za utalii.
Naye mwongoza utalii wa kujitegemea,Levis Lewis amesema vijana zaidi ya asilimia 70 Tanzania wamejiajiri kufanya kazi ya kuongoza utalii na kupitia sera hiyo inapingana na kile kinachofanyika kwa sasa kudaiwa leseni.
Amesema hadi sasa amefanyakazi ya utalii kwa miaka 35, hakuwahi kuona jambo la aina hiyo la kudaiwa leseni kwani waongoza utalii kipato chao ni kidogo na malipo yanayoainishwa kuyalipia ni mengi na suala la utalii ni la msimu.