Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imesema kuwa imewapa watumishi wake nafasi ya kuchagua ama kubaki TPA au kusitisha mkataba wa ajira na TPA na kuajiriwa na Kampuni ya DP World ya Dubai.
TPA imesema hayo katika taarifa yake ya ufafanuzi jana kuhusu hali ya ajira za watumishi wake katika Bandari ya Dar es Salaam na kueleza kuwa Machi 20, mwaka huu ilitoa taarifa kwa watumishi wake juu ya mabadiliko ya uendeshaji wa bandari hiyo, gati namba sifuri (RoRo) hadi gati namba saba.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa TPA katika taarifa yake ya Machi 20, mwaka huu watumishi walielekezwa kuwa mabadiliko hayo yamesababishwa na mkataba wake na Kampuni ya DP World ya Dubai kwa miaka 30 kuanzia Oktoba 22, mwaka jana.
“Kutokana na mabadiliko hayo katika usimamizi na uendeshwaji wa maeneo tajwa, watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam walitakiwa kuchagua ama kubaki TPA au kusitisha mkataba wa ajira na TPA na kuajiriwa na DP World papo hapo,” imefafanua taarifa hiyo.
TPA imeeleza kuwa Menejimenti ya mamlaka hiyo ilitoa taarifa hiyo kwa watumishi wake baada ya kukamilisha programu maalumu ya kuwaelimisha na kutoa ufafanuzi wa kina na taarifa sahihi juu ya mabadiliko hayo kwa watumishi wake.
Katika taarifa hiyo, ilielezwa kuwa watumishi watakaoridhia kujiunga na DP World walitakiwa kuwasilisha taarifa zao kabla au ifikapo Machi 29, 2024, huku wale wasiotaka kujiunga na DP World watabaki TPA kwa kuwa mamlaka itaendelea kuhitaji watumishi kwa ajili ya kutoa huduma katika bandari zake zinazoendelea kuboreshwa nchini.
TPA ilieleza kuwa taarifa hiyo ilitolewa kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kuhamisha huduma kwa DP World na kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuwathamini watumishi wake kwa kuzingatia maslahi ya pande zote husika kwa mujibu wa sheria ya nchi.