Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WATU wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kuingiza vifaa vya mawasiliano ya intaneti nchini bila kufuata utaratibu wa kisheria vyenye jina la STARLINK KIT/DEVICE.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 22, 2024 Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amewataja watu hao kuwa ni Claudian Makaranga (28) mkazi wa Kawe, Kinondoni na Hongliang Yang (35) Mchina, mkazi wa Kigamboni.
“Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na kikosi kazi maalum cha kuzuia na kupambana na matumizi ya makosa ya kimtandao limefanikiwa kuwakamata watu hao ambao wamekuwa wakijitangaza kuuza vifaa na kutoa huduma ya intaneti nchini kupitia mtandao ya kijamii wa Instagram kwa akaunti yenye jina la STARLINK.
“Baadhi ya vifaa vilivyoingizwa nchini imebainika vilishauzwa na kutumika katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam kitendo ambacho ni kosa na kinyume na sheria kwani havijaidhinishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Vifaa vilivyokamatwa ni Starline Dish 12, Starlink Router 12,” amesema.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kuwa makini na matumizi ya vifaa vya mawasiliano, ambavyo havijaidhinishwa na mamlaka husika.
Aidha Jeshi hilo pia limewakamata Wilfred Werandumi (44), Mkazi wa Tungi, Morogoro na Abdulrahim Mwakibinga (30), Mkazi wa Mwandege, Morogoro kwa tuhuma za kutumia majina ya Viongozi mbalimbali wa nchi kutapeli watu kwa kujifanya wanaomba michango ya harusi, misiba na matibabu.
“Baadhi viongozi ambao majina yao yametumika katika utapeli huu ni Dkt Stergomena Tax, Innocent Bashungwa, Mohamed Mchengerwa, Mhandisi Hamadi Masauni, na Katibu Mkuu wa zamani wa CCM Daniel Chongolo.
“Amekamatwa pia Salum Kingu (25) mkazi wa Mbalizi, Mbeya na Loveness Silonga (24) mkazi wa Mbalizi, Mbeya kwa tuhuma za kutumia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Facebook yenye jina la KOPA FASTER TULIA TRUST FOUNDATION na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali kwa kudai kuwa wanatoa mikopo kwa masharti nafuu na haraka wakitumia namba ya simu 0749 704445,” amesema.
Hata hivyo amesema Jeshi hilo linaendelea na ufuatiliaji mkali wa tabia hizi na watuhumiwa wote watashughulikiwa vikali kwa mujibu wa sheria.