Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma
Imeelezwa kuwa uwepo wa shughuli za kibinadamu na uwepo wa majanga ya asili vimetajwa kuwa ni moja ya sababu ya kuongezeka kwa kina cha maji katika Ziwa Tanganyika.
Hayo yamebainishwa kupitia mkutano wa mwaka wa kamati za kukabiliana na Majanga katika Mkoa wa Kigoma na mikoa jirani ya nchi ya Burundi uliofanyika katika Ukumbi wa NSSF Manispaa ya Kigoma Ujiji mjini Kigoma.
Kutokana na tafiti zilizofanywa zimeonesha kuwa, athari za majanga ya asili ikiwemo milipuko ya Volkano katika baadhi ya milima nchini Jamhuri ya Kimokrasia ya Kongo (DRC), husababisha lava iliyopoa pamoja na udongo kuingia katika mto Lukuga kisha kuzuia maji kupita kwa ufanisi na kuingia katika Bahari ya Atlantic.
Aidha kupitia kikao hicho, imebainishwa kuwa ongezeko la shughuli za kibinadamu pembezoni mwa Mto Lukuga zinasababisha mmomonyoko wa ardhi hivyo mchanga hujaa katika mto huo na kutoruhusu maji kupita kwa ufanisi kutoka ziwa Tanganyika ili kuingia baharini.
Baadhi ya athari za ongezeko la kina cha maji katika Ziwa Tanganyika ni maji kujaa katika maeneo yaliyojengwa miundombinu mbalimbali hususani bandari, makazi, kupotea kwa fukwe pamoja na baadhi ya mito inayoingiza maji ziwani humo kufurika na kuathiri mashamba na makazi.
Katika hatua nyingine wajumbe wa kikao hicho wameafikiana kuzishauri Serikali za Tanzania, Burundi na Congo DR kuweka mikakati mipya ya udhibiti wa shughuli za kibinadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika ziwa hilo na maeneo jirani ikiwemo kuongeza kasi katika kusimamia matumizi bora ya ardhi.
Aidha katika kukabiliana na majanga, kikao hicho kimebainisha changamoto zinazokinzana na juhudi za kufikia malengo ya kamati hizo ikiwemo ufinyu wa bajeti, ukosefu wa elimu ya kukabiliana na majanga kwa wananchi, uharibifu wa mazingira, uhamiaji haramu pamoja na matumizi hafifu ya teknolojia katika kukabili majanga.
Sambamba na hilo wajumbe hao wamependekeza serikali katika nchi hizo jirani kuzingatia mikakati ya pamoja iliyowekwa kwa ajili ya kukabiliana na majanga na kuishusha ngazi za chini za kiserikali ili iweze kutekezwa na wananchi ambao ndio walengwa.