Na Edward Kondela, JammhuriMedia, Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa wanawake wachakataji na wafanyabiashara wa mazao ya uvuvi barani Afrika wana mchango mkubwa katika Sekta ya Uvuvi, hususan katika uchatakaji na kilimo cha mwani.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi. Jovice Mkuchu, wakati akifungua kikao cha mtandao wa wanawake barani Afrika wanaochakata mazao ya uvuvi, kikiwa na lengo la kukuza uelewa kuhusu uongozi katika mitandao wanayoiwakilisha katika nchi zao.
Akimwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Bi. Mkuchu amesema, serikali inatambua umuhimu wa wanawake katika kuwezesha na kuendeleza Sekta ya Uvuvi barani Afrika, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiwezesha na kuinua wanawake kwenye kilimo cha mwani na shughuli za uvuvi.
Aidha, ameongeza kuwa Tanzania imefurahi kuwezesha kikao hicho cha siku tatu kinachodhihirisha namna inavyoshirikiana na nchi mbalimbali zikiwemo za Bara la Afrika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Mtandao wa Wanawake Afrika Wanaojishughulisha na Uchakataji na Biashara ya Samaki (AWFISHNET) wenye makao makuu nchini Tanzania Bi. Editrudith Lukanga, amebainisha kuwa mtandao huo una wanawake ambao ni viongozi wa mtandao kutoka nchi mbalimbali takriban 44.
Bi. Lukanga amesema kuwa mtandao huo ulianzishwa Mwaka 2017 kwa msaada wa Umoja wa Afrika (AU) kupitia Shirika la Umoja wa Afrika la Rasilimali za Wanyama (AU-IBAR), ambapo katika kikao hiki kinachofanyika nchini moja ya malengo makuu ni kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili wanawake katika Sekta ya Uvuvi.
Pia, amesema wanawake wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kukuza Sekta ya Uvuvi kwa kuwa asilimia 60 ya wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani baada ya samaki kuvuliwa ni wanawake.
Ameongeza kuwa mtandao huo unaangalia namna wanawake wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika kutatua changamoto, kuangalia katiba na mpango mkakati kwa kuwa na sauti moja barani Afrika na kumfanya mwanamke aweze kuthaminika katika hali inayotakiwa.
Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamesema wamekuwa wakipata elimu na kubadilishana mawazo kutoka nchi mbalimbali barani Afrika ili mtandao huo uwe na tija katika kukuza Sekta ya Uvuvi.
Wamebainisha kuwa baadhi ya changamoto za Sekta ya Uvuvi barani Afrika zimekuwa zikifanana hivyo itakuwa rahisi kwao kuwa na sauti ya pamoja katika kupata suluhu ya changamoto hizo.