Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Watu binafsi wamebainika kuchimba visima vya maji ambavyo vinatoa huduma kwa gharama ambazo hazibebeki kwa wananchi,ambapo imeibua changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma hiyo katika Jiji la Dar es salaam.
Ameyasema hayo leo Machi 20,2024 Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, katika viunga vya Makao Makuu ya mtandao huo Mabibo-Jijini Dar es Salaam,katika semina za Jinsia na maendeleo(GDSS).
Amesema wamebaini kufanyika biashara ya maji jambo ambalo si sawa kwani ni haki ya mtu na hitaji la msingi kwa binadamu hivyo hayapaswi kuuzwa wanatakiwa kuyapata bure.
“Maeneo ya nchi za wenzetu mtu akitaka maji anaenda tu bombani anakinga anakunywa akitaka ya chupa ni mapenzi yako,swala la kuwa na vizimba kwenye maeneo ya shule na ambayo watu wanaweza kuvifikia linatakiwa kutiliwa mkazo “. amesema
Aidha Bi.Lilian ameeleza kuwa baadhi ya vizimba vya maji vimevamiwa na watu wasio na mapenzi mema kwa nchi ambapo ameomba mamlaka husika kuondoa watu hao ili kufufua vizimba hivyo ili wananchi waondokane na kadhia hiyo.
Kwa Upande wake, Diwani kata ya Makurumla Manspaa ya Ubungo Bw. Bakari Kimwanga ameahidi kwenda katika eneo lake na kupambana kutatua changamoto hiyo kwa kuzungumza na viongozi wa juu kuunda nguvu za pamoja kuondoa tatizo hilo.
Nae,Mwenyekiti Msaidizi kata ya Majohe, akiwakilisha Wilaya ya Ilala Bw.Joseph Safari amesema kundi kubwa linaloathirika katika suala la maji ni wanawake ambapo upatikanaji wa huduma hiyo unakadiliwa kuwa ni zaidi ya masaa manne kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
“Tunatamani kujua serikali imewekeza nguvu yao kiasi gani kwenye maji kwa kuzingatia taarifa na takwimu, tunatamani kuona uwazi wa tafiti ambazo serikali imefanya, ikizitolea majibu ni kiasi gani maji yameingia kwenye jamii,na suala la mifumo ya maji safi yaliyopita katika njia ya bomba la maji taka ambapo yakipasuka tunakunywa maji ambayo yamechanganyika na majitaka,tunatamani kupata majibu”. mmesema safari.
Maji yamekuwa ni changamoto endelevu hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na ongezeko la watu nchini katika maeneo ya mjini na vijijini,ambao wanakadiriwa kuwa zaidi ya milioni 60.