Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera
Serikali ya Awamu ya Sita imetoa kiasi cha Sh bilioni 431 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya barabara za kimkakati, ili kuhakikisha Mkoa wa Kagera unaunganisha barabara zake na mikoa mingine nchini na nchi za Afrika Mashariki.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Ntuli Mwaikosesy akielezea miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, amesema kati ya fedha hizo kiasi cha Sh bilioni 37 kimetumika kufanya matengenezo ya barabara za ndani na ujenzi wa madaraja, huku Sh bilioni 13 zikitumika katika miradi midogo ya barabara.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu idadi ya wakandarasi wazawa wanaotekeleza miradi mikubwa na midogo mkoani Kagera imeongezeka, huku ajira za kudumu na vibarua ambao wameajiriwa kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia ikifikia 3,000.
Amesema mtandao wa barabara za lami mkoani umeongezeka, miradi yote ya zamani ambayo ilikuwa imekwama imekamilika kwa asilimia 100 ikiwemo kuunganisha kilometa 50, barabara ya Nyakanazi, Kabingo hadi Kakonko ,ambayo inaunganisha Mkoa wa kigoma na Kagera.
Pia amesema taa za barabarani zilizowekwa ndani ya miaka mitatu ni 486 huku taa 578 zikitarajiwa kuendelea kuwekwa katika miji yote midogo na maeneo yaliyochangamka, ili kuimarisha uchumi wa wananchi pamoja na kuwezesha ufanyaji biashara mchana na usiku.
Amesema miradi ya barabara za kimkakati inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ambayo itaufungua Mkoa wa Kagera katika sekta za kilimo , mifugo, biashara na utalii ikiwemo kuuunganisha mkoa wa Kagera na mikoa mingine na nchi jirani.
Miradi hiyo ni barabara ya Lusahunga hadi Rusumo, barabara ya Bugene hadi hifadhi ya Taifa ya Burigi, Chato, barabara ya Nkwenda hadi Kaisho, barabara ya Kagera Sugar Junction hadi Kakunyu na mradi wa upanuzi wa barabara ya njia nne ya Bukoba .
“Ndani ya miaka mitatu mengi yamefanyika wananchi wamelipwa fidia sasa tunaunganisha mkoa wetu na mikoa mingine na nchi jirani ili kuufungua kiuchumi, ajira nyingi, wakandarasi wazawa wameaminika na wanaendelea na kazi zao, miradi mingine mikubwa inaendelea na usanifu, “amesema Mwaikosesy.