Timu ya soka Alliance ya jijini Mwanza, inayoundwa na wachezaji wenye umri chini ya miaka 11, imetwaa ubingwa wa mashindano yaliyozishirikisha nchi tisa.
Nchi hizo ni Sudan, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Nigeria, Zambia, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Alliance imetwaa ushindi katika kundi A lililoshirikisha timu za wachezaji wenye umri chini ya miaka 11, kwa kuifunga Zambia mabao 3-1 katika fainali iliyochezwa jijini Kampala, Uganda, hivi karibuni.
Ushindi huo umeiwezesha Alliance kutwaa kombe na medali ya dhahabu, huku mchezaji wake, Mustapha Ally, akitwaa nafasi ya mchezaji bora wa mashindano hayo.
Pia timu ya Alliance inayoundwa na wachezaji wenye umri chini ya miaka 15 imeshika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Kampala bao 1-0 katika mchezo wa fainali.
Katibu Mkuu wa Shule ya Soka ya Alliance ya jijini Mwanza, Kessy Mziray, amesema ushindi huo ni matokeo ya mazoezi ya kutosha na uongozi mzuri wa shule hiyo.
Alliance imekuwa ikifanya ziara mara kwa mara ndani na nje ya nchi kucheza na timu mbalimbali na kutwaa ubingwa katika mashindano mengi.
Mkurugenzi wa shule hiyo, James Bwire, ameanzisha timu hiyo kuibua na kuendeleza watoto wenye vipaji vya soka sambamba na kuwaendeleza kielimu wawe wachezaji mahiri watakaoiwezesha Tanzania kumudu ushindani wa soka barani Afrika kama si duniani.